October 15, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TRA yapongezwa kwa makusanyo ya kodi

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

KAMATI ya Kudumu ya Bajeti ya Bunge imeipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuvuka malengo ya ukusanyaji wa kodi kupitia mifumo ya kidijitali na kuimarisha ushirikiano na walipakodi.

Akizungumza Dodoma wakati wa semina kuhusu mifumo ya IDRAS, TANCIS na uondoshaji mizigo bandarini, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mashimba Ndaki, alisema mafanikio ya TRA yanachangia juhudi za Tanzania kujitegemea kiuchumi.

Amesema katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027, TRA ilikusanya Sh trilioni 10.65, sawa na asilimia 107.49 ya lengo la Sh trilioni 9.91.

Ndaki amesema mifumo ya kidijitali na elimu ya kodi vimeimarisha ukusanyaji wa mapato, akiahidi kuwa wabunge watakuwa mabalozi wa mifumo hiyo ili kusaidia Serikali kupata fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo.

Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Juma Mwenda, amesema matumizi ya mifumo ya kidijitali yameongeza uwazi, kuboresha usimamizi wa kodi na kupunguza mawasiliano ya ana kwa ana kati ya watumishi wa TRA na walipakodi.

Amesema idadi ya walipakodi nchini imefikia milioni tisa, huku TRA ikisajili walipakodi wapya zaidi ya 447,000 katika robo hiyo.

Ameahidi kuendelea kuboresha huduma na kutatua changamoto za walipakodi kwa wakati.


Naye Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, anesema kufungwa kwa mashine za skana katika mipaka yote kutasaidia kudhibiti upotevu wa mapato na kuongeza ufanisi katika ukaguzi wa mizigo.