

Na Joyce Kasiki, Rukwa
MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imesema imeendelea kuongeza fursa za kiuchumi kwa vijana kupitia usajili wa makundi maalumu na utoaji wa zabuni za umma, huku ikiwataka vijana nchini kutumia fursa hizo kujikwamua kiuchumi.
Mkurugenzi wa Kuendeleza Uwezo, Winifrida Samba, alisema hayo kwa niaba ya Mkuruhenzi Mkuu wa Mamlaka hoyo Denis Simba,wakati akizungumza mbele ya Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda, alipotembelea banda la mamlaka hiyo katika maadhimisho ya Wiki ya Vijana mkoani Rukwa.
Samba amesema ushirikiano kati ya PPRA na Ofisi ya Rais inayoshughulikia maendeleo ya vijana, pamoja na kuingizwa kwa suala la usajili wa makundi maalumu , ajenda ya Mwenge imechangia kuongeza idadi ya makundi yaliyosajiliwa na kupanua fursa za vijana kushiriki katika ununuzi wa umma.
Amesema kabla ya juhudi hizo, kulikuwa na jumla ya makundi maalumu 1,557, yakiwemo makundi ya vijana 878, huku idadi hiyo ikiongezeka kufuatia hatua mbalimbali zilizochukuliwa kuhamasisha usajili.
Kwa mujibu wa takwimu alizowasilisha, kuanzia April Mosi hadi Oktoba 10 mwaka huu, idadi ya makundi maalumu yaliyosajiliwa ilikuwa imefikia 31,928 yakiwemo makundi ya vijana 15,165.
Katika hatua nyingine, Samba amesema kuanzia Julai 2023 hadi Oktoba 10 mwaka huu ni makundi 33,482 kati ya hayo makundi ua vijana ni 16,549 ambapo , jumla ya zabuni 3,466 zilitolewa kwa makundi maalumu, zikiwa na thamani ya Sh bilioni 74.32.
Amefafanua kuwa katika zabuni hizo, makundi ya vijana yalipata mikataba 2,066 yenye thamani ya Sh bilioni 40.6, hatua inayodhihirisha mchango wa ununuzi wa umma katika kuwawezesha vijana kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
Amesema PPRA itaendelea kusimamia ununuzi wa umma ili kuhakikisha unakuwa endelevu na unawanufaisha wananchi kiuchumi na kijamii, hususan vijana na makundi mengine maalumu.
“Tunawahimiza vijana kuendelea kutumia fursa zinazopatikana katika ununuzi wa umma kwa kujiandaa na kushiriki katika zabuni zinazotolewa na taasisi za umma,” amesema Samba.
Amesema ushiriki wa makundi maalumu katika zabuni za umma ni miongoni mwa njia zinazoweza kuwasaidia vijana kupata mikataba, kukuza shughuli zao za biashara na kuongeza mchango wao katika maendeleo ya Taifa.
Akitembelea banda hilo, Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda, ameipongeza PPRA kwa shughuli inazofanya, ikiwamo juhudi za kuwawezesha vijana na makundi maalumu kunufaika na fursa zinazotokana na ununuzi wa umma.

More Stories
Mwenge wakagua miradi ya bilioni 14, wakabidhiwa Rukwa.
Kikwete atangaza Mkutano wa Rasilimaliwatu Afrika
AHF yatumia uwezeshaji kupunguza VVU