October 5, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vijana 50 Tanga kudhibiti uchafuzi

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Tanga

SERIKALI ya Mkoa wa Tanga imeanzisha operesheni maalumu ya kukabiliana na uchafuzi wa mazingira kwa kuunda kikosi kazi cha vijana 50 kitakachopewa jukumu la kutoa elimu,kufuatilia utekelezaji wa sheria za mazingira na kuwakamata watakaobainika kutupa taka ovyo, huku faini ya kosa hilo ni kuanzia sh.50,000.

Hatua hiyo ni sehemu ya mpango mpya wa mkoa huo wa kufanya usafi wa mazingira kuwa zoezi endelevu kuanzia ngazi ya kaya, mitaa na vijiji, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Buriani, amesema kikosi hicho kitashirikiana na Halmashauri na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuhakikisha sheria ndogo za mazingira zinatekelezwa kwa vitendo.

Akizindua Msaragambo Maalumu wa kila mwezi uliopewa jina la “Balozi Dkt. Batilda Mazingira Day,” Dkt. Buriani amesema kikosi hicho kitakuwa na jukumu la kubaini maeneo yenye changamoto za usafi, kutoa elimu na maelekezo kwa wananchi, huku wanaokaidi maagizo na kuendelea kuchafua mazingira wakichukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Amesema kikosi hicho hakitakuwa juu ya sheria na kabla ya kuanza kazi wanachama wake wataapa kutopokea rushwa wala kutumia nguvu katika utekelezaji wa majukumu yao, huku makusanyo yote ya faini yakifanyika kupitia mfumo rasmi wa ukusanyaji mapato kwa kutumia mashine za POS na kutolewa risiti.

“Hatukusudii kutoza faini kwa wananchi, tunakusudia kuboresha mazingira yetu. Tutahakikisha kosa linathibitishwa na hatua zinachukuliwa kwa mujibu wa sheria,” amesema Dkt. Buriani.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, kikosi hicho kitakaguliwa na kutambuliwa rasmi na NEMC kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Tanga ili kiweze kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria, ikiwemo kuchukua hatua dhidi ya watakaokiuka kanuni za mazingira.

Dkt. Buriani amezitaka Halmashauri zote 11 za Mkoa wa Tanga, chini ya usimamizi wa Wakuu wa Wilaya, kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa ufanisi na wananchi wanashirikishwa katika kulinda mazingira yao kwa hiari.

Amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa Tanga ni miongoni mwa mikoa inayotoa mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa, ikichangia takribani Sh6 bilioni kwa mwezi katika pato la Taifa na kushika nafasi ya sita kitaifa, hivyo maendeleo hayo yanapaswa kwenda sambamba na mazingira safi na salama.

Awali akimwakilisha Mkurugenzi wa NEMC Kanda ya Kaskazini, Meneja wa NEMC Kanda ya Bagamoyo, Ndimbumi Mboneke, amesema kila mwananchi ana wajibu wa kuhakikisha mazingira yanayomzunguka yanakuwa safi na salama, sambamba na kutoa taarifa kwa mamlaka husika anapobaini uharibifu wa mazingira.

Mboneke amesema sheria ya mazingira inampa kila Mtanzania haki ya kuishi katika mazingira safi na salama, lakini pia inamweka katika wajibu wa kushiriki katika kuyatunza, akitoa wito kwa wananchi kuiga mfano wa Mohamed Hilal, mkazi wa Tanga aliyekabidhiwa cheti maalumu cha shukrani na NEMC kwa mchango wake katika kuhamasisha utunzaji wa mazingira.

Wakati huo huo, Meya wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Mustafa Selebos amesema,halmashauri hiyo iko tayari kutekeleza maagizo ya mkoa, akitangaza kuanza kwa operesheni ya kuondoa wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga waliopanga biashara zao katikati ya stendi ya daladala.

Amesema kuanzia sasa usafi maalumu utafanyika kila tarehe moja ya mwezi, huku vibanda na miundombinu inayochangia uchafuzi na kuziba maeneo ya stendi ikiondolewa.
“Yale yote uliyoelekeza kwetu sisi ni amri, si ombi. Kuanzia sasa tutafanya usafi maalumu kila tarehe moja ya mwezi,” amesema Selebos.