October 5, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nyamanoro kupata  zahanati baada ya miaka

Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online,Mwanza

LICHA ya kuwa moja  ya kata iliopo mjinj ndani ya Halmshauri  ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza,wananchi wa Kata ya Nyamanoro kwa muda mrefu wamekabiliwa na changamoto ya ukosefu wa huduma za afya za Serikali katika kata na mitaa yao.

Hali hiyo sasa imeanza kupata ufumbuzi baada ya Serikali kuanza ujenzi wa zahanati katika kata hiyo, hatua inayolenga kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.

Akizungumza na TimesMajira Online katika mahojiano maalumu Mjumbe wa Mtaa wa Nyamanoro Mashariki Kata ya Nyamanoro Teresia Rogati amesema, ujenzi huo ni faraja kwa wakazi wa mitaa ya  Nyamanoro Mashariki, Kilimahewa, Nenetwa na Mkudi, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitegemea vituo vya afya  binafsi.

Amesema,kwa sasa wananchi wanasubiri hatua ya uwekaji paa na umaliziaji wa jengo hilo, huku akieleza kuwa kukamilika kwake kutawasaidia kupata huduma kwa wakati bila kulazimika kwenda maeneo ya mbali.

Rogati amesema,baadhi ya wananchi wamekuwa wakifuata huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure, hali ambayo imewahi kusababisha wagonjwa kuchelewa kupata huduma, huku baadhi ya wanawake wakijifungua njiani.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyamanoro Mashariki, Missa Budundu amesema, ujenzi huo unaendana na sera ya Serikali ya kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.Na kwa sasa wakazi wa kata hiyo hutegemea huduma kutoka maeneo ya Iloganzala, Kirumba na Buzuruga, hivyo zahanati hiyo itakapokamilika itapunguza adha ya kutumia muda na nauli kwenda kata nyingine.

Budundu amesema,eneo ilipojengwa zahanati hiyo ni la milimani, ambako kuna idadi kubwa ya wananchi, hivyo wakazi wa maeneo  hayo watakuwa wamesogezewa huduma ya qmatibabu karibu na makazi yao.

Diwani wa Kata ya Nyamanoro,Abdulrahman  Kange amesema,baada ya kuingia madarakani alibaini kuwa afya ni miongoni mwa changamoto kubwa, hivyo akaifanya kuwa kipaumbele chake cha kwanza.

Amesema,ujenzi huo unatekelezwa kwa mapato ya ndani  ya halmshauri hiyo na tayari  kiasi cha sh.milioni 40 zimetumika, huku jengo likiwa limefikia hatua ya renta na likisubiri fedha kwa ajili ya hatua zinazofuata.

Kange amesema,mahitaji ya huduma hiyo ni makubwa kutokana na jiografia ya kata hiyo  kuwa ni milimani na idadi ya wananchi wanaofikia 24,624, ambao kwa sasa baadhi hulazimika kwenda Hospitali  ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure kufuata huduma.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Dkt.Maria Kapinga amesema,lengo la Serikali ni kusogeza huduma kwa wananchi ili wasiende umbali mrefu kufuata huduma,ambapo zahanati ya Nyamanoro  inatarajiwa kuhudumia wananchi 24,624 na kutoa huduma za OPD, vipimo, chanjo, kliniki ya baba, mama na mtoto, uzazi wa mpango, ushauri nasaha na kujifungua.

Amesema,kituo hicho kitakuwa na matabibu watatu, wauguzi wanne, mtaalamu mmoja wa dawa na mmoja wa maabara, huku huduma zote zikitolewa kupitia mfumo wa GoTHOMIS.

 Naye Mkuu wa Divisheni ya Mipango na Uratibu, Deogratius Lukomanya amesema, ujenzi umefikia asilimia 43 baada ya kupokea shilingi milioni 40 kati ya milioni 150 zilizotengwa, na unatarajiwa kukamilika Juni 2027 kulingana na upatikanaji wa fedha.

“Zahanati ya  Nyamanoro jengo la wagonjwa  wa nje(OPD),boma limekamilika na ujenzi ukihusisha boma,matundu ya vyoo,shimo lamkutupia taka,majivu na kondo la nyuma kupitia fedha za mapato ya ndani ya halmshauri,”amesema Lukomanya.