October 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uwekezaji wa Michezo wavutia Watalii Tanzania

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

“Sikufikiri Tanzania kuwa ni ya kisasa kiasi hiki.” Huo ni mshangao wa mwandishi wa habari na mtengeneza maudhui kutoka kutoka nchini Ufaransa, Alizee Morat, baada ya kutembelea Tanzania katika ziara inayolenga kuangazia maandalizi ya AFCON na fursa za utalii.

Alizee , ambaye amewahi kutembelea nchi mbalimbali za Afrika, ikiwemo Cameroon, amesema amevutiwa na miundombinu ya Uwanja wa Benjamin Mkapa utaokatumika kwenye mashindano, na ukarimu wa Watanzania, akisema uzoefu wake nchini umekuwa tofauti na matarajio yake.

Ziara hiyo ni sehemu ya mkakati wa Tanzania kutumia AFCON kama jukwaa la kuitangaza nchi kimataifa, huku kundi la watu mashuhuri, waandishi wa habari na watengeneza maudhui likitembelea maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari, Afisa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Nassor Garamatatu, amesema kundi hilo limekuja kujionea maandalizi ya Tanzania na kutumia vyombo vyao vya habari pamoja na majukwaa ya kidijitali kuufahamisha ulimwengu kuhusu utayari wa nchi.

Wageni hao wametembelea Uwanja wa Benjamin Mkapa na Uwanja wa Gymkhana utakaotumika kwa ajili ya mazoezi wameeleza kuridhishwa na uwekezaji uliofanyika katika miundombinu ya michezo.

Kwa mujibu wa Garamatatu, kupitia ziara hiyo Tanzania inalenga kupata matangazo ya kimataifa yatakayosaidia kuwafikia watalii na wadau wa michezo kutoka sehemu mbalimbali duniani.

“Mbali na Dar es Salaam, kundi hilo linatarajiwa kutembelea Arusha na Fumba Zanzibar, likilenga kujionea vivutio na maandalizi ya AFCON, “ amesema.

Kiongozi wa msafara huo, John Jackson, amesema Wizara ya Maliasili na Utalii imeamua kutumia umuhimu wa AFCON kuwaunganisha wageni hao na vivutio vya Tanzania ili watumie majukwaa yao kuitangaza nchi.

Jackson amesema walifurahishwa na Uwanja wa Benjamin Mkapa, wakilinganisha uwekezaji wake na viwanja vikubwa duniani.