October 3, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Utalii wa Arusha wanusa fursa mkutano wa IPU

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

SEKTA ya utalii inatarajiwa kunufaika kwa kiasi kikubwa na ujio wa wajumbe wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), unaotarajiwa kufanyika Jijini Arusha kuanzia Oktoba 5 hadi 9, 2026, huku mamia ya wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani wakitarajiwa kutumia muda wao kutembelea vivutio vya utalii kabla au baada ya mkutano huo.

Mkutano huo unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC), unatarajiwa kuwakutanisha takribani washiriki 2,000 kutoka mabunge 183, hali inayotoa fursa kwa kampuni za utalii, waongoza watalii, hoteli na watoa huduma wengine katika sekta hiyo kuongeza shughuli zao na kutangaza vivutio vya Arusha na Tanzania kwa wageni wa kimataifa.

Kwa wafanyabiashara wa utalii, ujio wa wajumbe hao si fursa ya kupata mapato pekee wakati wa mkutano, bali pia ni nafasi ya kuwafahamisha wageni kuhusu vivutio mbalimbali vya utalii vinavyopatikana Arusha na maeneo mengine ya Tanzania, hivyo kuongeza uwezekano wa baadhi yao kuongeza siku za kukaa nchini.

Mkurugenzi wa kampuni ya utalii ya Viola, Violet Mfuko, amesema sekta ya usafiri na utalii inatarajiwa kupata ongezeko la mahitaji kutokana na wageni wanaohitaji usafiri kutoka uwanja wa ndege kwenda hotelini, AICC na maeneo mbalimbali ya jiji pamoja na kutembelea vivutio.

Amesema hali hiyo inatoa nafasi kwa kampuni za utalii na watoa huduma za usafiri kutumia mkutano huo kujitangaza na kujenga mahusiano ya kibiashara na wageni wanaofika Arusha.

Kwa upande mwingine, sekta ya malazi inatarajiwa kuongezeka kwa shughuli kutokana na mahitaji ya vyumba vya hoteli, huku migahawa na watoa huduma za chakula wakipata nafasi ya kuwahudumia wageni hao na kuwaonesha bidhaa na vyakula vya asili vya Tanzania.

Mmoja wa watoa huduma za chakula, Juliana John, anayefanya shughuli hiyo katika eneo la Bondeni, amesema mkutano huo ni fursa kwa wafanyabiashara kutumia bidhaa za ndani na kuonesha ubora wa vyakula vya Kitanzania kwa wageni wa kimataifa.

Amesema wageni wanapopata fursa ya kuonja vyakula vya asili na kuona bidhaa zinazozalishwa nchini, wanaweza kuwa sehemu ya soko la bidhaa hizo hata baada ya kurejea katika nchi zao.

Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Dk. Toba Nguvila, amewataka wadau wa sekta binafsi kutumia fursa hiyo kwa kutoa huduma bora na kuhakikisha jiji linakuwa tayari kuwahudumia wageni watakaofika kwa ajili ya mkutano huo.

Dk. Nguvila amesema ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kuhakikisha mikutano mikubwa ya kimataifa inakuwa na manufaa kwa wananchi, hususan wafanyabiashara wanaotoa huduma zinazohitajika na wageni.

Mbali na utalii, mkutano huo unatarajiwa kuongeza shughuli katika sekta za usafiri, chakula, malazi na afya, kutokana na mahitaji yatakayozalishwa na idadi kubwa ya wajumbe na wageni watakaokuwepo jijini.