Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
TANZANIA inaendelea kutumia fursa ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kujitangaza kimataifa kupitia kampeni ya Destination Tanzania, ambapo imewaalika wanahabari na watengeneza maudhui kutoka mataifa mbalimbali kuja kujionea vivutio vya utalii, utamaduni na maandalizi ya Tanzania kuelekea michuano hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa kuwapokea wanahabari na watengeneza maudhui kutoka Marekani, Canada, Afrika Kusini, Ufaransa na Uingereza.
Amesema ziara hiyo ya siku saba inalenga kuwawezesha wageni hao kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii pamoja na kuona maandalizi yanayofanyika kuelekea AFCON, ili kutumia majukwaa yao kufikisha ujumbe kuhusu Tanzania katika masoko ya kimataifa.

“Kupitia ziara hii, Tanzania inalenga kutumia ushawishi wa wanahabari na watengeneza maudhui hawa kufikisha ujumbe kuhusu utalii, michezo, utamaduni na fursa nyingine zilizopo nchini kwa hadhira kubwa nje ya Tanzania,” amesema Dkt. Abbas.
Katika mazungumzo yake na wageni hao, Dkt. Abbas amewaalika kurejea nchini kwa mara nyingine ili kushuhudia na kutangaza mashindano ya AFCON pamoja na uzoefu wa Tanzania kama mwenyeji.

Kwa upande wake, John Jackson, Mtanzania aliyehusika kuwaalika wageni hao nchini, amesema ziara hiyo inalenga kuwawezesha kuifahamu Tanzania kwa karibu na kupata uzoefu wa moja kwa moja utakaowawezesha kutengeneza maudhui yenye kuvutia kwa hadhira zao.
“Wageni hawa katika kipindi cha siku saba watatembelea maeneo mbalimbali ya utalii, ikiwamo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro na Zanzibar, huku pia wakipata fursa ya kuona miundombinu ya michezo,” amesema Jackson.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Dkt. Theresa Mugobi, amesema kampeni ya Destination Tanzania inalenga kuongeza uelewa kuhusu vivutio na fursa mbalimbali za utalii zilizopo nchini.

Amesema ushiriki wa wanahabari na watengeneza maudhui katika kutangaza Tanzania unaweza kusaidia kufikisha ujumbe wa utalii katika masoko mbalimbali kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Wageni hao ni Sara Poraria kutoka Canada, Karina Bermudez kutoka Marekani, Geneefah Lee kutoka Afrika Kusini, Alizee Morat kutoka Ufaransa, pamoja na Adam Britton na Cameroon James kutoka Uingereza.



More Stories
Ubunifu wa teknolojia kuongeza ajira na uchumi
Utalii wa Arusha wanusa fursa mkutano wa IPU
Wachimbaji wadogo Geita wapatiwa leseni tatu mpya