Na Joyce Kasiki, Geita

WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) umetangaza fursa mbili za uwekezaji katika maeneo ya Bishota na Msigiti mkoani Geita, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kushiriki katika miradi ya ujenzi kupitia mfumo wa ubia kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP).
Meneja Mawasiliano na Masoko wa TBA, Adam Mwingira, amesema hayo katika maonyesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini mkoani Geita eneo la Misheni Kota lina ukubwa wa takribani mita za mraba 10,600 na limeandaliwa kwa ajili ya uwekezaji, huku eneo la Msikiti likiwa miongoni mwa maeneo mengine yanayotarajiwa kuendelezwa.
Mwingira amesema TBA inaendelea kutangaza fursa za uwekezaji katika maeneo 38 yaliyopo Tanzania Bara, huku taasisi hiyo ikilenga kuwavutia wawekezaji kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Amesema katika eneo la Bishota, TBA inatarajia kujenga majengo ya makazi yenye jumla ya nyumba 12, yatakayokuwa na takribani ghorofa sita, zikiwa na nyumba zenye vyumba vitatu, viwili na kimoja.
Kwa mujibu wa Mwingira, TBA pia imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi nchini, ikiwemo nyumba za viongozi, majengo ya makazi kwa watumishi wa umma na wananchi wengine, pamoja na miundombinu ya afya.
Ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Chato na Hospitali ya Geita, ambazo zinatoa huduma kwa wananchi, huku TBA pia ikiwa imeshiriki katika ujenzi wa nyumba za viongozi, ikiwemo nyumba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Aidha, amesema TBA imekuwa mshauri wa Serikali katika miradi ya majengo, ikiwemo jengo la Serikali lililopo Chamwino, ambapo taasisi hiyo ilihusika katika usanifu na usimamizi wa ujenzi.
Mwingira pia ametoa shukrani kwa wadau waliotembelea banda la TBA wakati wa maonesho ya madini, pamoja na wale waliofuatilia shughuli za taasisi hiyo kupitia mitandao ya kijamii.
Amesema TBA imepata nafasi ya pili katika kundi la taasisi za umma zilizoshiriki maonesho hayo, akieleza kuwa tuzo hiyo ni matokeo ya ushirikiano wa wadau mbalimbali na uongozi wa taasisi hiyo.
TBA imewataka wananchi na wawekezaji kuendelea kufuatilia taarifa za fursa na shughuli zake kupitia njia mbalimbali za mawasiliano na mitandao ya kijamii ya taasisi hiyo.

More Stories
GF yakabidhi magari kwa wachimbaji, yaongeza huduma
Homera ampongeza Rais Samia upatikanaji wa Umeme
DIB yasisitiza umuhimu wa Bima ya Amana