October 3, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ESAP Mining yang’ara tuzo tatu maonesho ya madini



Na Joyce Kasiki, Geita


KAMPUNI ya ESAP Mining Services Limited inayojishughulisha na masuala ya madini ,imepata mafanikio makubwa katika Maonyesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika mkoani Geita baada ya kushinda tuzo tatu katika vipengele mbalimbali.


Kampuni hiyo ilitwaa tuzo ya Mdhamini Mkuu wa Maonyesho, Kampuni Bora ya Uchorongaji Miamba (Drilling), huku ikishika nafasi ya pili katika kipengele cha Kampuni Bora ya Uchimbaji Madini.


Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo hizo leo Oktoba 2, 2026, katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita, Afisa Utawala na Mawasiliano wa ESAP Mining Services Limited, Shabani Sadiki, amesema utambuzi huo umeongeza hamasa kwa kampuni hiyo kuendelea kuboresha huduma zake.


Sadiki amesema tuzo hizo pia zimeipa kampuni hiyo nguvu ya kuendelea kuwekeza katika matumizi ya teknolojia za kisasa na kubuni mbinu mbalimbali zitakazoongeza ufanisi katika shughuli za uchimbaji na utoaji wa huduma kwa wadau wa sekta ya madini.


“Tunachukulia tuzo hizi kama hamasa ya kuendelea kuboresha huduma zetu, kutumia teknolojia za kisasa na kutafuta mbinu mpya zitakazoongeza ufanisi katika kazi tunazofanya,” amesema.


Aidha, Sadiki ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweka sera, sheria na kanuni zinazohimiza ushiriki wa Watanzania katika shughuli za kiuchumi kupitia mfumo wa ushirikishwaji wa wazawa (Local Content).


Amesema utekelezaji wa sera hiyo umeendelea kutoa nafasi kwa kampuni za Kitanzania kushiriki katika uwekezaji na kutoa huduma mbalimbali ndani ya sekta ya madini, jambo linaloongeza fursa za ushiriki wa wazawa katika shughuli za kiuchumi.


Pamoja na hayo, aliwashukuru viongozi na wafanyakazi wa Esap Mining Services Limited kwa mchango wao katika kufanikisha mafanikio hayo, huku akitambua pia ushirikiano unaotolewa na kampuni na wadau mbalimbali wanaofanya nao kazi.


Sadiki amesema ushirikiano kati ya kampuni zinazotoa huduma katika shughuli za uchimbaji, wawekezaji na wachimbaji wadogo ni muhimu katika kuimarisha sekta ya madini na kuongeza fursa za biashara kwa kampuni za Kitanzania.


Kwa upande wake, mafanikio yaliyopatikana na Esap Mining Services Limited katika maonyesho hayo yanaendelea kuonyesha umuhimu wa teknolojia, ubunifu na ushirikiano wa wadau katika kuongeza uwezo wa kampuni za Kitanzania zinazotoa huduma katika sekta ya madini.