October 2, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ESAP yaongoza huduma vilipuzi, uchimbaji Afrika Mashariki

Na Joyce Kasiki, Geita

KAMPUNI inayojihisisha na usambazaji wa vilipuzi  na uchorongaji  (ESAP Mining Services) imeendelea kupanua huduma zake za usambazaji wa vilipuzi na uchorongaji (drilling services) katika sekta ya madini nchini Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki, huku ikiwekeza katika teknolojia na uzalishaji wa ndani.

Kampuni hiyo, inayoongozwa na Mkurugenzi Mhandisi Yahya Ruyaga, inajieleza kuwa kampuni ya kizalendo inayomilikiwa kwa asilimia 100 na Watanzania na yenye uwezo wa kusambaza vilipuzi na kutoa huduma za uchorongaji kwa migodi mikubwa pamoja na wachimbaji wadogo na wa kati.

“Kwa sasa, ESAP inatoa huduma katika migodi ikiwamo Bulyanhulu (Buckreef), Shanta Mining, Siam Gold (Samagold) na Nyanzaga, ambako pia inatoa huduma za uchorongaji. Kampuni hiyo pia imekuwa ikihudumia wachimbaji wadogo na wa kati, hususan katika Ukanda wa Ziwa.”Amesema Mhandisi Ruyaga

Ruyaga amesema utekelezaji wa sera ya Maudhui ya Ndani (Local Content) umechangia kampuni hiyo kuongeza uwekezaji katika teknolojia na uwezo wa uzalishaji nchini.

Amesema ESAP imewekeza katika kiwanda kilichopo Wilaya ya Bukombe kinachozalisha vimiminika vya vilipuzi (emulsion), pamoja na magari maalum yenye teknolojia ya kuchanganya vilipuzi katika eneo la kazi.

Kwa mujibu wa Ruyaga, kampuni hiyo pia inaendelea na mazungumzo na kampuni za nje kwa ajili ya kupata mashine ndogo za kisasa zitakazowawezesha wachimbaji wadogo wanaofanya uchimbaji wa chini ya ardhi kupata bidhaa na huduma kwa gharama nafuu zaidi.

Amesema uwekezaji huo unalenga kuongeza ufanisi katika shughuli za uchimbaji na kupanua upatikanaji wa teknolojia kwa wachimbaji wadogo.

Ruyaga amewashukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Madini na watendaji wa Wizara ya Madini kwa kuweka mazingira aliyoyataja kuwa wezeshi kwa uwekezaji katika teknolojia na kukuza maudhui ya ndani katika sekta ya madini.

Mhandisi Ruyaga alikuwa akizungumza na waandishi wa habari katika banda la kampuni hiyo wakati wa maonnesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini Mkoani Geita.