Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Kigoma
WANANCHI 344 kati ya 346 waliofika katika zoezi la “disclosure” mtaa wa Mgeo, Kata ya Buhanda mkoani Kigoma, wameridhia fidia zao na kusaini fomu za kuthibitisha uhakiki wa taarifa zao za mali zinazohusika na mradi wa SGR.
Mthamini Mwandamizi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rashid Mageta amesema,wananchi hao ni sehemu ya wananchi 370 waliofanyiwa uthamini katika eneo hilo.
Amesema hadi sasa wananchi 346 wamefika kuhakiki taarifa zao, ambapo 344 wameridhia fidia na kusaini fomu za uhakiki huku wawili wakieleza kutoridhishwa na fidia walizoainishiwa,lakini wananchi 24 kati ya 370 waliofanyiwa uthamini bado hawajafika kuhakiki taarifa zao.
Pia amesema,zoezi hilo bado linaendelea ili kuwapa fursa wananchi 24 ambao hawajafika kushiriki katika uhakiki wa taarifa zao na kutoa hoja pale wanapoona kuna taarifa zinazohitaji marekebisho au ufafanuzi.
Hivyo amewahimiza hao ambao bado hawajafika kushiriki katika zoezi hilo ili kuhakiki taarifa zao na kuhakikisha taarifa zao zinakuwa sahihi kabla ya hatua zinazofuata za mchakato wa mradi wa SGR.
Mageta amesisitiza,kuwa ushiriki katika zoezi la “disclosure” ni hatua muhimu katika mchakato wa uthamini, kwa kuwa humpa mwananchi fursa ya kuona na kuhakiki taarifa za mali yake pamoja na taarifa zinazohusiana na fidia.
Ameongeza kuwa wananchi wanaohusika wanapaswa kutumia fursa hiyo kuhakiki taarifa zao na kutoa hoja kwa wakati, hatua inayosaidia kubaini na kushughulikia changamoto mapema kabla ya kukamilika kwa mchakato wa uthamini na ulipaji wa fidia.

More Stories
Wananchi Kigoma wasisitizwa kuhakika taarifa za mali
Dkt.Homera awasili Wizara ya Nishati
Nimekuja kuiunganisha timu ya maendeleo si kutawala:Magomi