October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Muheza watakiwa kujihadhari na mvua

Na Steven William,TimesMajira Online. Muheza

SERIKALI ya Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, imetoa tahadhari kwa wakazi wilayani hapa kuondoa michanga na udongo katika mitaro ya kupitisha maji kwenye mitaa wanayoishi, ili kujihadhari na mvua kubwa pindi itakapoanza kunyesha.

Hayo yamesemwa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mhandisi Mwanasha Tumbo wakati akizungumza na wananchi katika Uwanja wa Jitegemee.

Amesema wakazi wote wanaoishi wilayani hapa, lazima waweke tahadhari kusafisha mitaro ya kupitisha maji katika mitaa, wanayoishi, ili pindi mvua kubwa itakapoanza wasipate mafuriko.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema wakazi wa mji wa Muheza, waliojenga nyumba zao katika mabonde ya kupitisha maji waanze kuhama kwenda kwenye nyumba ambazo zipo juu kwa kuwa mafuriko, hayawezi kufika huko atakayekaidi atachukuliwa hatua.

Mwanasha amesema wafanyabiashara wote walioweka maduka katika maeneo ya mabondeni, waanze kuondoka na wanaoishi nyumba mbovu pia wahame ili kusitokee watu kupata hasara ama maafa.