Na Mwandishi wetu, TimesmajiraOnline,Mbeya
MSANII wa kizazi kipya, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, amesema miaka kumi ya Taasisi ya Tulia Trust imeonesha ubunifu na uwezo wa uongozi wa mwanzilishi wa taasisi hiyo, Dkt. Tulia Ackson.
Diamond ameyasema hayo alipoungana na Dkt. Tulia kumkabidhi nyumba Grace Deya, mwenye umri wa miaka 70, mkazi wa Tembela jijini Mbeya, ambaye amejengewa nyumba hiyo na Taasisi ya Tulia Trust kutokana na hali yake duni ya maisha na kukosa makazi bora.
Msanii huyo amemsifu Dkt. Tulia, ambaye pia ni Mbunge wa Uyole, kwa kutumia ubunifu wake kuwagusa wananchi bila kujali mipaka ya eneo lake la uongozi.
“Tunasikia kila mahali hapa nchini unawagusa wananchi. Wananchi wa Jimbo la Uyole mmepata kiongozi ambaye majimbo mengine wanamtamani awe wao. Naomba tumlinde, tumtetee na pia tumtie moyo,” amesema Diamond.
Akizungumzia nyumba hiyo, Dkt. Tulia amesema katika kipindi cha miaka kumi tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Tulia Trust, taasisi hiyo inajivunia kumkabidhi nyumba ya kuishi mwananchi huyo mwenye uhitaji.
Amesema nyumba hiyo ni ya 26 kujengwa na taasisi hiyo kwa ajili ya wananchi wenye uhitaji katika kipindi cha miaka kumi.
“Nyumba hizi tumezijenga katika maeneo mbalimbali ndani ya Mkoa wetu wa Mbeya. Sisi tumejenga nyumba, nawaomba ninyi wengine kama mnaweza, nendeni mkawape chochote mlicho nacho, hata chakula,” amesema Dkt. Tulia.
Akizungumzia mafanikio ya miaka kumi ya Taasisi ya Tulia Trust, Dkt. Tulia amesema taasisi hiyo imefanya shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo kugharamia bima za afya kwa kaya zisizojiweza, kutoa vifaa na kugharamia masomo kwa wanafunzi wenye uhitaji, pamoja na kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu.


More Stories
Briquettes yaibua fursa kupunguza gharama nishati kupikia
Wananchi Arusha wapokea kwa hamasa Mkutano wa IPU
Paradise Mission yawabeba kielimu vijana 100 wa mazingira magumu