September 28, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Paradise Mission yawabeba kielimu vijana 100 wa mazingira magumu

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mbeya

ZAIDI ya vijana 100 waliotoka katika mazingira magumu wamefanikiwa kuendelea na elimu ya juu katika vyuo na taasisi mbalimbali nchini kupitia ufadhili wa masomo.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Awali na Msingi Paradise Mission, Rozalina Mtumbuka, amesema hayo Septemba 26, 2026, wakati wa mahafali ya tano na maadhimisho ya miaka mitano tangu kuanzishwa kwa shule hiyo.

Mtumbuka amesema vijana hao wamepata fursa ya kuendelea na elimu katika taasisi mbalimbali, ikiwemo Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), pamoja na vyuo vilivyopo Zanzibar na Dodoma.

Kwa mujibu wa Mtumbuka, fursa hiyo imetokana na ufadhili unaotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa shule hizo, Ndele Mwaselela, kwa lengo la kuwawezesha vijana kutoka katika mazingira magumu kuendelea na elimu, kujitegemea na kujenga maisha yao.

“Katika kipindi cha miaka mitano, zaidi ya vijana 100 wamepata fursa ya kuendelea na elimu katika vyuo mbalimbali kupitia ufadhili wa Mkurugenzi wa shule hii. Aidha, shule imeendelea kurejesha kwa jamii kwa kuchangia katika sekta za elimu, maji, barabara na uwekaji wa taa,” amesema.

Amesema pamoja na kutoa elimu ya kitaaluma, shule hiyo imekuwa ikiwajengea wanafunzi uwezo katika stadi mbalimbali za maisha, ikiwemo ushonaji, mapishi na ujuzi mwingine unaoweza kuwasaidia kujitegemea.

Mtumbuka amesema juhudi hizo ni sehemu ya kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu inayowawezesha kukabiliana na changamoto za maisha na kutumia ujuzi wanaoupata kwa manufaa yao na jamii kwa ujumla.

Mgeni Rasmi katika Mahafari hayo ,Baba Paroko ,Olivarius Kalupale amesema kuwa elimu ni gharama hivyo wazazi wanapaswa kulitambua hilo katika kuhakikisha kuwa wanawasimamia watoto wao kielimu.

“Elimu ni gharama ndugu zangu wapeni fursa ya kusoma ,msomeshe mtoto wako katika sehemu iliyo sahihi ikiwa ni pamoja na hapa Paradise Mission kwani licha ya elimu wanayopata watoto hawa lakini wanamtanguliza Mungu “amesema.