Na Joyce Kasiki, Geita
MENEJA wa Benki ya Azania Tawi la Geita Rhoda Baluhya amesema ,Benki hiyo imeweka mkazo katika kuwawezesha wadau wa sekta ya madini, wafanyabiashara na wawekezaji kupata mitaji kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao, ikiwamo mikopo ya hadi Sh.5 bilioni kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa dhahabu.
Baluhya ametoa kauli hiyo leo Septemba 27, 2026, alipokuwa akozinhumza mbele ya Naibu Waziri wa Madini Dkt.Steven Kiruswa wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.
Amesema ,hatua hiyo inalenga kuwasaidia wachimbaji na wafanyabiashara wa dhahabu wanaouza madini yao kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambapo mteja anaweza kupata mkopo bila dhamana kwa sharti la kutumia akaunti ya Benki ya Azania.
Benki hiyo imeeleza kuwa inaweza kutoa hadi asilimia 80 ya thamani ya fedha zinazotarajiwa kupokelewa na mteja, hatua inayolenga kuwawezesha wadau wa mnyororo wa thamani wa madini kuendelea na shughuli zao wakati wakisubiri kukamilika kwa taratibu za malipo.
Mbali na mikopo kwa sekta ya madini, Azania inatoa huduma mbalimbali za kifedha kwa wafanyabiashara na wawekezaji, zikiwamo mikopo ya mitaji, uwekezaji pamoja na ununuzi wa mitambo na vifaa vya uzalishaji.
Kwa mujibu wa Baluhya , mikopo ya mitaji hutolewa kwa ajili ya kuendesha shughuli za biashara na inaweza kulipwa kwa vipindi vya miezi mitatu, huku mikopo ya uwekezaji ikilenga utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Aidha amesema , benki hiyo inatoa mikopo kwa ajili ya ununuzi wa mitambo na vifaa vya uzalishaji, ikiwamo mashine, vifaa vya kutengeneza betri na vifaa vingine vya viwandani.
Huduma hiyo pia inahusisha mikopo kwa ajili ya ununuzi wa vyombo vya usafirishaji, vikiwamo magari, malori na matipa, kwa ajili ya kuwawezesha wafanyabiashara na wawekezaji kuongeza uwezo wa uendeshaji wa shughuli zao.
Katika hatua nyingine, Benki ya Azania imesema imeingia makubaliano na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ya kutoa mikopo yenye riba ya asilimia tano kwa mwaka kwa ajili ya ujenzi wa vituo na maeneo ya huduma za mafuta vijijini.
Kwa mujibu wa benki hiyo, mpango huo unalenga kuongeza upatikanaji wa nishati na kuchochea shughuli za uzalishaji katika maeneo ya vijijini, hususan maeneo yanayozunguka shughuli za uchimbaji madini.
Benki hiyo pia inatoa mikopo ya uwekezaji ya muda mrefu inayoweza kufikia miaka minane, kwa ajili ya ununuzi wa vifaa, magari na mahitaji mengine muhimu kwa wawekezaji katika sekta ya madini.
Kwa mujibu wa Azania, mikopo hiyo inalenga kuwawezesha wawekezaji kuongeza uwezo wa uzalishaji na kuendesha shughuli zao kwa ufanisi zaidi.
i.

More Stories
Wakazi Kahama kunufaika na huduma za mawasiliano
Kamati ya serikali yakagua miundombinu kuelekea AFCON 2027
Equity Bank yaongeza nguvu sekta ya Madini Tanzania