September 27, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BRELA yawahamasisha wafanyabiashara kusajili biashara na nembo

Na Joyce Kasiki, Geita

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umewahamasisha wafanyabiashara na wajasiriamali wanaoshiriki Maonesho ya Tisa ya Madini mkoani Geita kutumia fursa hiyo kupata elimu na huduma za usajili wa biashara, majina ya biashara, kampuni na nembo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la BRELA kwenye maonesho hayo, Afisa wa BRELA, Salum Makuka, amesema wakala huo umeweka huduma zake katika maonesho hayo ili kuwafikia wananchi kwa urahisi na kuwawezesha kupata elimu pamoja na huduma za usajili papo hapo.

Makuka amesema huduma zinazotolewa na BRELA ni pamoja na usajili wa kampuni, majina ya biashara, nembo za biashara (trademarks), viwanda vidogo, leseni za biashara za Daraja A pamoja na usajili na ulinzi wa bunifu kupitia hati miliki (patent).

Amesema wananchi wanaofika katika banda hilo kwa ajili ya kupata huduma za usajili hawatozwi gharama za urahisishaji wa huduma, isipokuwa hulipa ada rasmi ya Serikali inayohusika na huduma wanayoomba.

“Tumeleta huduma hizi hapa ili wananchi wapate elimu na pia waweze kusajili biashara zao papo hapo. Urahisishaji wa kupata huduma ni bure, isipokuwa wananchi watalipa ada ya Serikali,” amesema Makuka.

Amesema usajili wa biashara ni muhimu kwa mfanyabiashara kwa kuwa taasisi mbalimbali, ikiwamo benki na taasisi za fedha, huhitaji mfanyabiashara kuwa na usajili halali anapohitaji huduma kama mikopo au kushiriki zabuni.

Makuka pia ameonya kuwa kuendesha biashara bila kusajili jina la biashara kunaweza kumuweka mfanyabiashara katika hatari ya kupoteza haki ya kutumia jina alilolijenga kwa muda mrefu endapo mtu mwingine atalitangulia kulisajili.

“Unaweza kuanzisha biashara kwa juhudi kubwa, lakini mtu mwingine akaja na kusajili jina hilo. Hivyo ni muhimu kuhakikisha jina la biashara limesajiliwa ili kulinda biashara yako,” amesema.

Aidha, amesema usajili wa biashara una umuhimu katika mipango ya Serikali ya kutambua sekta mbalimbali zinazochangia uchumi, ikiwamo sekta ya madini, kwa kuwa taarifa za wafanyabiashara waliosajiliwa zinaweza kusaidia Serikali katika kupanga na kutoa huduma, motisha au fursa mbalimbali za maendeleo.

Makuka alisema BRELA itaendelea kutoa huduma katika maonesho hayo hadi tarehe 3, akiwataka wananchi kutumia fursa hiyo kupata elimu kuhusu mfumo mpya wa BRELA unaojulikana kama BOS, unaowawezesha kufanya huduma mbalimbali kwa njia ya mtandao.

Amesema wananchi wanaweza kupata elimu ya namna ya kufungua akaunti, kuingia katika mfumo, kufanya usajili wa biashara, pamoja na kutekeleza matakwa ya kisheria kama kuwasilisha taarifa za mwaka (annual returns) na kulipia ada za uendelezaji wa majina ya biashara.

Kwa upande wake, mfanyabiashara kutoka Nayubi Cosmetics amesema BRELA imewasaidia kupata uelewa zaidi kuhusu usajili wa biashara na nembo.

Mfanyabiashara huyo amesema mwaka uliopita alifanikiwa kusajili jina la biashara kupitia BRELA, lakini hakuwa akifahamu umuhimu wa kusajili nembo ya biashara.

Amesema baada ya kufika katika maonesho hayo mwaka huu, alipata elimu zaidi kutoka kwa maafisa wa BRELA na kusaidiwa kukamilisha taratibu za kuongeza usajili unaohusiana na biashara yake.

Amesema huduma hiyo imemsaidia kupata uelewa wa mahitaji ya kisheria katika uendeshaji wa biashara na namna ya kulinda jina pamoja na utambulisho wa biashara yake.

BRELA imeendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara na wajasiriamali katika maonesho hayo huku ikiwataka wananchi kutumia fursa hiyo kupata huduma za usajili .