September 27, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watoto waathirika wa moyo, jamii yatakiwa kutambua dalili

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online,Mwanza

JAMII imetakiwa kuongeza uelewa kuhusu magonjwa ya moyo kwa watoto, kwani baadhi yao huchelewa kugundulika kutokana na dalili kuchukuliwa kuwa ni za magonjwa mengine, ikiwemo pneumonia.

Akizungumza na majira juzi Daktari wa Moyo wa Watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Dkt.Julieth Kabirigi amesema,Maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani, yanayofanyika Septemba 29 kila mwaka, ni muhimu katika kuikumbusha jamii kutunza afya ya moyo na kutambua dalili za magonjwa hayo mapema.

Dkt.Kabirigi amesema,matatizo ya moyo hayawaathiri watu wazima pekee, bali pia watoto, huku akieleza kuwa kwa mujibu wa tafiti, kati ya watoto 1,000 wanaozaliwa, watoto kati ya wanane hadi 10 huzaliwa wakiwa na changamoto ya moyo,hali hiyo inaonesha umuhimu wa kuongeza elimu na huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa watoto.

Amesema katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, kwa mwezi wanaweza kuwaona watoto kati ya 200 hadi 250 wanaofika kliniki kwa ajili ya uchunguzi wa matatizo ya moyo,kati yao takribani asilimia 10 hadi 20 hubainika kuwa na changamoto za moyo, hali inayohitaji uchunguzi na ufuatiliaji wa kitaalamu.

Pia amesema,uelewa kuhusu dalili za magonjwa ya moyo kwa watoto bado ni mdogo, jambo linalosababisha baadhi yao kutibiwa mara kwa mara kama wagonjwa wa “pneumonia”,ambapo dalili zinazopaswa kupewa uzito kuwa ni mtoto kuugua mara kwa mara, kushindwa kupumua vizuri, kutokwa jasho kupita kiasi na kutokuongezeka uzito.

Daktari huyo amewataka wazazi na walezi kuwapeleka watoto hospitalini mapema wanapoona dalili hizo, hasa katika hospitali zenye huduma za moyo kwani uchunguzi wa mapema unaweza kusaidia kubaini tatizo na kuwezesha mtoto kupata matibabu na ufuatiliaji unaohitajika kwa wakati.

Kwa upande wa chanzo, amesema baadhi ya matatizo ya moyo huanzia wakati wa kuzaliwa na yanaweza kuhusishwa na urithi au vinasaba,pia maambukizi ya rubella wakati wa ujauzito, hasa katika hatua za mwanzo, matumizi ya baadhi ya dawa bila ushauri wa kitaalamu na dawa za kulevya vinaweza kuongeza uwezekano wa mtoto kuzaliwa akiwa na changamoto ya moyo.

Amesema matatizo yanaweza pia kujitokeza baada ya mtoto kuzaliwa kutokana na magonjwa mbalimbali, ikiwemo homa ya baridi yabisi (rheumatic fever), inayoweza kuathiri valvu za moyo,pia mtoto anaweza kupata “myocarditis” yaani uvimbe au maambukizi yanayoathiri misuli ya moyo, hali inayoweza kupunguza uwezo wa moyo kusukuma damu vizuri.

Dkt. Kabirigi amesema madhara ya magonjwa hayo yanaweza kumfanya mtoto ashindwe kucheza, kwenda shule na kushirikiana na watoto wenzake, huku baadhi yao wakikabiliwa na utapiamlo na moyo kushindwa kufanya kazi vizuri hivyo alisisitiza umuhimu wa elimu kwa wazazi, walezi na watoa huduma za afya ili watoto wenye dalili waweze kufikishwa hospitalini mapema.

Aidha, Dkt. Kabirigi ameiomba Serikali kuhakikisha huduma za bima ya afya zinawafikia wananchi wote, akisema hatua hiyo itasaidia kurahisisha upatikanaji wa matibabu kwa watoto na watu wengine wanaohitaji huduma za afya. Alisisitiza kuwa wananchi wasisite kwenda hospitalini wanapoona dalili za ugonjwa, ili waweze kupata uchunguzi, ushauri na matibabu kwa wakati.