Na Joyce Kasiki, Geita
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Sangu, amewataka wachimbaji wadogo nchini kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kupitia Hifadhi Scheme ili kupata kinga dhidi ya majanga na changamoto za maisha ya baadaye.
Sangu ametoa wito huo leo Sept 24,2026 wakati akizungumza katika banda la NSSF kwenye Maonyesho ya Tisa ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita, akisema wachimbaji wadogo ni miongoni mwa kundi linalolengwa na mpango huo wa hifadhi ya jamii.
Amesema Hifadhi Scheme imeanzishwa kwa ajili ya watu waliojiajiri ambao awali hawakuwa na fursa ya kupata huduma za hifadhi ya jamii, akiwamo mama lishe, waendesha bodaboda na wachimbaji wadogo.
“Leo wana nguvu ya kufanya kazi na kuwepo mgodini, lakini kesho wanaweza kupata majanga; atakayekuwa kimbilio lao ni NSSF kupitia Hifadhi Scheme,” amesema Sangu.
Waziri huyo pia ameipongeza NSSF kwa kushiriki katika maonyesho hayo, akisema ushiriki wake unaonyesha kutambua umuhimu wa Sekta ya Madini katika uchumi wa nchi na mchango wake katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2050.
Amesema katika dira hiyo, Sekta Binafsi inatarajiwa kuchangia asilimia 70, Serikali Kuu asilimia 22 na Mashirika ya Umma asilimia nane, hivyo Sekta Binafsi kuwa injini muhimu ya utekelezaji wa dira hiyo.
Sangu amesema NSSF, ambayo kwa mujibu wa Sheria ya mwaka 2018 imepewa jukumu la kusimamia Sekta Binafsi, imeonyesha kutambua nafasi ya Sekta ya Madini kwa kushiriki katika maonyesho hayo.
Aidha, amesema NSSF imeweka lengo la kufikisha thamani ya mfuko huo Sh trilioni 24 ifikapo mwaka 2031 kupitia Mpango Mkakati wa Miaka Mitano.
Kwa mujibu wa Sangu, mwaka 2022 NSSF ilikuwa na thamani ya Sh trilioni 5.7, huku hadi Desemba mwaka jana thamani hiyo ikiwa imefikia Sh trilioni 10.4.
Amesema kwa sasa thamani ya mfuko huo imefikia Sh trilioni 11.5 na inatarajiwa kuzidi Sh trilioni 12 ifikapo Desemba mwaka huu.
Sangu pia amewapongeza waajiri katika Sekta ya Madini wanaowasilisha michango ya wafanyakazi wao katika mifuko ya hifadhi ya jamii, akitolea mfano makampuni makubwa ya madini kama Geita Gold Mining Limited (GGML).
Amesema utii wa sheria katika kuwasilisha michango ya wafanyakazi ni muhimu katika kuhakikisha wanapata stahiki zao za hifadhi ya jamii.
Kwa upande wake, Meneja Mawasiliano wa NSSF, Lulu Mengele, amesema thamani ya mfuko huo imefikia Sh trilioni 11.5.
Sangu pia aliupongeza uongozi wa Mkoa wa Geita kwa kutoa fursa kwa NSSF kushiriki katika maonyesho hayo na kuwataka viongozi wa mfuko huo kuendeleza kasi ya kuongeza wanachama.
Amesema Meneja wa NSSF Geita amepewa lengo la kusajili wanachama 5,000 na tayari amefikia zaidi ya nusu ya lengo hilo, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha lengo hilo linafikiwa ndani ya mwaka huu.

More Stories
Visima vya umwagiliaji vyawakomboa wakulima wadogo
PSSSF yapongezwa kwa mafanikio makubwa
Miradi ya kusambaza umeme vitongojini kukamilika ifikapo 2030