Na Joyce Kasiki, Geita
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, ameeleza mafanikio yaliyopatikana na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), akisema mfuko huo umeendelea kuimarisha huduma kwa wanachama na wastaafu.
Sangu ameyasema hayo leo Sept 24 ,2026 wakati akizungumza katika banda la PSSSF kwenye Maonyesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita, ambapo ameeleza kuwa PSSSF imefanya jitihada mbalimbali kuhakikisha wastaafu wanaandaliwa vizuri kwa maisha ya baada ya utumishi.
Amesema moja ya maeneo ambayo mfuko huo umeweka mkazo ni utoaji wa elimu kwa wastaafu kwa kushirikiana na waajiri, hatua inayolenga kuwasaidia wanachama kujiandaa mapema kwa maisha baada ya kustaafu.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa, thamani ya mfuko imeendelea kukua kutoka Sh trilioni 7.4 wakati Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani hadi kufikia Sh trilioni 16.96, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya mara mbili.
Sangu pia amesema PSSSF imeendelea kuboresha huduma za malipo kwa wastaafu, ambapo mfuko huo hulipa mafao ya wastaafu kwa wakati, huku pensheni za kila mwezi zikilipwa kabla ya tarehe 25 ya kila mwezi.
Aidha, amesema kima cha chini cha pensheni kwa mwezi kimeongezwa kutoka Sh 100,000 hadi Sh 250,000, hatua inayolenga kuboresha hali ya wastaafu wanaopokea pensheni hiyo.
Katika hatua nyingine, Waziri Sangu amesema PSSSF imeboresha mifumo yake ya TEHAMA, jambo ambalo limewezesha huduma mbalimbali kufanyika kwa urahisi zaidi.
Amesema kwa sasa uhakiki wa wastaafu unaweza kufanyika kwa urahisi bila kuwalazimu kusafiri, hivyo kupunguza usumbufu na gharama zinazoweza kujitokeza katika upatikanaji wa huduma.
Sangu amesisitiza umuhimu wa wananchi kupata elimu kuhusu huduma zinazotolewa na PSSSF, ikiwemo mafao na maandalizi ya maisha baada ya kustaafu.

More Stories
Sangu awataka wachimbaji wadogo kujiunga NSSF
Visima vya umwagiliaji vyawakomboa wakulima wadogo
Miradi ya kusambaza umeme vitongojini kukamilika ifikapo 2030