Na Joyce Kasiki, Geita

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amewataka waajiri kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa kisheria kwa kujisajili katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na kuwasilisha michango kwa wakati.
Waziri Sangu ametoa agizo hilo leo Sept 24,2026 baada ya kutembelea banda la WCF katika Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, mkoani Geita.
Katika ziara hiyo, Waziri alipata maelezo kuhusu shughuli zinazotekelezwa na WCF, ikiwemo utoaji wa elimu kwa waajiri na wafanyakazi kuhusu haki na taratibu za kupata fidia pale mfanyakazi anapopata madhara kutokana na ajali au mazingira ya kazi.
Sangu ameeleza kuwa uzingatiaji wa taratibu za WCF ni muhimu zaidi katika sekta zenye mazingira hatarishi, ikiwemo uchimbaji wa madini, ambako wafanyakazi hukabiliwa na changamoto mbalimbali zinazoweza kuathiri usalama na afya zao.
Amesisitiza pia umuhimu wa waajiri kuhakikisha michango ya WCF inawasilishwa kwa wakati, hatua inayowezesha wafanyakazi na wategemezi wao kupata stahiki pale yanapotokea mazingira yanayostahili fidia kwa mujibu wa taratibu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa WCF, Dkt. John Mduma, alisema taasisi hiyo imeendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa kutumia mifumo ya kidigitali, hatua inayowawezesha waajiri kufanya usajili na malipo kwa njia ya mtandao bila kulazimika kufika ofisini.
Mduma pia ameeleza kuwa huduma hizo zimeendelea kusogezwa karibu na wananchi kupitia teknolojia za simu, huku WCF ikiendelea kutumia maonesho hayo kuwaelimisha wadau kuhusu huduma, wajibu wa waajiri na haki za wafanyakazi.

More Stories
Sangu awataka wachimbaji wadogo kujiunga NSSF
Visima vya umwagiliaji vyawakomboa wakulima wadogo
PSSSF yapongezwa kwa mafanikio makubwa