Na Mwandishi Wetu,,TimesMajira
WAJASIRIAMAILI wakiwemo Mama Lishe katika Wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma wameshauriwa kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na badala yake kuanza kutumia nishati safi ya kupikia ili kulinda afya zao na mazingira.
Ushauri huo umetolewa na Meneja Fedha wa Kampuni ya Oryx Gas Ashery Mbasha aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo Iman Mtafya katika hafla ya kukabidhi mitungi ya gesi 600 na vifaa vyake vilivyotolewa na kampuni hiyo kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo ambaye pia ni Waziri wa Katiba na Sheria Dk.Juma Homera.
Amesema ili kufikia lengo la Serikali angalau Watanzania asilimia 80 waweze kutumia nishati safi ifikapo mwaka 2034 ni vema jitihada za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia zikaendelea na Oryx Gas wamekuwa mstari wa mbele katika kampeni hiyo.
“Wilaya ya Namtumbo kama yalivyo maeneo mengine hapa nchini imekuwa na changamoto ya matumizi makubwa ya kuni na mkaa kwa muda mrefu na ndio kimekuwa chanzo kikubwa cha uharibifu wa misitu na iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa zitasababisha athari kubwa ikiwemo mabadiliko ya tabia ya nchi kama mnavyoona .

“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikisha kila Mtanzania anatumia nishati safi. Sisi kama tumeanza na ninyi Mama Lishe kwa sababu nyinyi ndio mnaotumia kuni nyingi zaidi na ndio mnaoathirika zaidi na moshi,” alisema
Amesisitiza matumizi ya gesi ya kupikia yatasaidia kupunguza kasi ya ukataji miti, kuboresha afya za wananchi kwa kupunguza moshi majumbani, kuokoa muda wa kupika na kuongeza ubora wa maisha kwa ujumla.

Mbasha amesema dhamira ya Oryx Gas ni kuhakikisha Tanzania inafikia mabadiliko kamili ya matumizi ya nishati safi ya kupikia. Wilaya ya Namtumbo ni moja ya maeneo ambayo tumeyawekea kipaumbele katika safari hii muhimu.
Pia ametoa rai kwa wananchi wa Namtumbo hasa waliopata mitungi ya gesi ya Oryx kutumia majiko hayo kwa usalama na kuendelea kueneza elimu ya matumizi ya gesi ya LPG katika jamii zenu. Kwa pamoja tunaweza kujenga Namtumbo yenye mazingira bora, afya bora na maendeleo endelevu.
Awali Mbunge wa Jimbo la Namtumbo ,ambaye pia ni waziri wa Katiba na sheria Dk.Juma Homera ameishukuru kampuni ya Oryx kwa kuwapatia majiko hayo na kueleza Dk.Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara wa nishati safi ya kupikia amekuwa akisisitiza utumiaji wa nishati safi nchini.
Dk.Homera amewataka wananchi kuunga mkono jitihada hizo za Rais na Serikali ya Awamu ya Sita kwa vitendo huku akiipongeza Oryx gas kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakiutoa kwa wananchi wa Namtumbo.

Kwa upande wake Mama Lishe Anifa Mahela amepongeza mpango huo mzuri wa kutoa elimu na kugawa bure mitungi kwa wajasiriamali huku akiiomba Serikali na wadau kama Oryx kuwasaidia kupata mitungi ya gesi na majiko ya nishati safi kwa bei ya ruzuku kutokana na mtaji mdogo walionao.

More Stories
Tanzania yapeleka wanajeshi 74 kulinda Amani Lebanon
Watatu wafariki,44 wajeruhiwa katika ajali wakitoka kuzika
Wakulima wa Mwani Zanzibar kunufaika huduma za kidijitali