September 18, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania yapeleka wanajeshi 74 kulinda Amani Lebanon

Na Mwandishi wetu,TimesMajira

TANZANIA imepata uteuzi wa kikundi cha Polisi Jeshi kitakachohudumu chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa katika kundi la 34/36 mwaka 2026, kwa ajili ya kutekeleza jukumu la ulinzi wa amani nchini Lebanon.

Uteuzi huo umetajwa kuwa ni ishara ya kuaminiwa kwa Tanzania na jumuiya ya kimataifa kutokana na mchango wake katika shughuli za kulinda amani duniani.

Hayo yamebainishwa jana jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Wanamaji, Rear Admiral Ameir Ramadhani Hassani, kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Jacob John Mkunda, wakati wa hafla ya kukabidhi bendera ya Taifa kwa kikundi hicho baada ya kumaliza mafunzo ya ulinzi wa amani yaliyofanyika katika Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania.

Mafunzo hayo yalianza Julai 2026 na kufungwa rasmi Agosti 28, mwaka huu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rear Admiral Hassani amesema Tanzania imeendelea kushirikiana na jumuiya ya kimataifa katika shughuli za kulinda amani, jambo linaloonesha mchango wa nchi hiyo katika juhudi za kudumisha amani duniani.

Amesema kutokana na uzoefu wa Tanzania katika operesheni za kulinda amani, vikundi viwili kutoka Benchi ya 35 na 36 vimechaguliwa kushiriki katika jukumu hilo nchini Lebanon.

“Kutokana na uzoefu wa Tanzania katika operesheni za kulinda amani, vikundi viwili kutoka Benchi ya 35 na 36 vimechaguliwa kushiriki katika jukumu hilo nchini Lebanon,” amesema.

Amesema jumla ya wanajeshi 74 wanatarajiwa kwenda Lebanon kutekeleza jukumu hilo.

Rear Admiral Hassani amewapongeza wanajeshi hao kwa kuchaguliwa na kuwataka watakapofika Lebanon kufuata maelekezo na taratibu za Umoja wa Mataifa, pamoja na kuwa tayari kufanya kazi na watu kutoka mataifa mbalimbali.

“Katika Umoja wa Mataifa kuna mataifa mengi ambayo tunafanya nayo kazi kwa pamoja, hivyo tuna imani kwa watu ambao tumewateua kwenda kutuwakilisha Tanzania wataenda kufanya kazi bila kubagua mataifa,” amesema.

Aidha, amewataka kusimamia kwa ukaribu taratibu za Umoja wa Mataifa na kutekeleza majukumu yao kwa utii, uhodari, uaminifu na nidhamu.

Amesema mchango wa Tanzania katika shughuli za kulinda amani katika nchi mbalimbali ni mkubwa, akibainisha kuwa ushiriki huo umeifanya nchi kuendelea kushirikiana na mataifa mbalimbali na kuaminiwa na Umoja wa Mataifa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kikundi hicho, Luteni Kanali Amulike Kabale, amesema kukabidhiwa bendera ya Taifa ni ishara ya imani na dhamana kubwa waliyopewa pamoja na taifa kwa ujumla.

Amesema kikundi chake kiko tayari kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia miongozo na maelekezo yote yaliyotolewa.

“Kukabidhiwa bendera hii ni imani na dhamana kubwa kwetu kwamba tumeaminiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na taifa kwa ujumla”amesema

Ameongeza kuwa kikundi hicho kitafanya kazi kwa kuzingatia misingi ya haki, utu wa kibinadamu, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali inayotolewa na Umoja wa Mataifa.

Luteni Kanali Kabale amesisitiza kuwa watatekeleza jukumu hilo kwa weledi, uaminifu, nidhamu, utii na ujasiri ili kuhakikisha bendera ya Taifa inarejea nchini ikiwa na heshima ya juu.

“Nawaahidi kuwa tutaitumikia bendera hii kwa heshima na uaminifu, na tutarudi nayo ikiwa na heshima ya hali ya juu kuwakilisha vyema Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na taifa kwa ujumla,” amesisitiza.

Naye mshiriki, Sajinitaji Irene Ntembo, amesema anajisikia furaha kubwa kupata nafasi hiyo na kwamba atatekeleza wajibu wake kwa kuzingatia miongozo, kanuni na taratibu zilizowekwa na Baraza la Umoja wa Mataifa pamoja na zile za kijeshi za Tanzania.

Amesema nidhamu ya hali ya juu, utii, uhodari na uaminifu vitakuwa msingi wa utendaji wake katika kutekeleza jukumu hilo.