Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online, Kigoma
MKOA wa Kigoma umejipanga kufikisha upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa asilimia 85 kwa wananchi waishio vijijini na asilimia 95 kwa wananchi waishio mijini ifikapo Desemba 2020.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA) mkoani Kigoma Mhandisi Mathius Mwenda amesema hivi sasa hali ya upatikanaji maji imepanda kutoka asilimia 56 ya mwaka 2015 hadi asilimia 67 kwa vijijini na asilimia 58 ya mwaka 2015 hadi asilimia 75.
Mhandisi Mwenda amesema jumla ya miradi 31 imetekelezwa na kukamilika, ambapo kupitia Mpango wa Malipo kwa Matokeo (PbR) miradi imekamilika na jumla ya vituo vya kuchotea maji 523 vinahudumia wananchi, na kupitia Programu ya Matokeo (PforR) mpango ulikua kutekeleza miradi 19, ambapo 18 ilikuwa ya ukarabati na utanuzi, na mmoja mpya. Kati ya miradi hiyo mitano imekamilika na inatoa huduma kwa wananchi, na utekelezaji wake umefanikishwa na wataalamu wa Wizara ya Maji kupitia utaratibu wa force account.
Aidha, Mhandisi Mwenda ameainisha kuwa wataalamu hao wanaendelea kukamilisha idadi ya miradi ya maji 10 inayotumia fedha za Mfuko wa Maji wa Taifa (NWF). Pamoja na hayo, baadhi ya miradi inatekelezwa kwa ushirikiano na Washirika wa Maendeleo, ikiwamo serikali ya Ubelgiji, Umoja wa Mataifa na Shirika la Water Mission na Islamic Foundation. Miradi inayoendelea kutekelezwa inatarajiwa kukamilika Desemba 2020 itaongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza kwa wakazi wa mkoa wa Kigoma.
Mkoa wa Kigoma unaundwa na wilaya sita ambazo ni wilaya ya Kigoma, Kasulu, Kibondo, Kakonko, Uvinza na Buhigwe.
More Stories
Benki ya Equity Tanzania yasaini mkataba wa kuwawezesha wanawake kiuchumi
Rais Samia alivyoguswa kifo cha msanii Grace Mapunda
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta