September 15, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kairuki: TTCL yafunguka, Tanzania yaingia kwenye Mapinduzi ya Kidijitali

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, amesema matumizi ya teknolojia ya kidijitali yamekuwa muhimu katika biashara, elimu na utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam baada ya kutembelea Kituo Jumuishi cha TTCL cha huduma za faiba Kijitonyama, Kairuki amesema Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa miaka 10 wa mageuzi ya kidijitali, ikiwamo kuongeza upatikanaji wa vifaa vya kisasa.

Amesema Tanzania imefikia asilimia 47 ya matumizi ya simu janja, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kuelimishwa kuhusu huduma za kidijitali zinazotolewa na kampuni za mawasiliano.

Kairuki pia amesema TTCL imepiga hatua katika huduma ya Faiba Mlangoni Kwako (FTTH), ikiwamo kuunganisha huduma hiyo na teknolojia za Smart Home.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, amesema shirika hilo lina maungio takribani 330,000 ya faiba na wateja wapatao 115,000, huku likilenga kufikisha maungio 750,000 ifikapo Juni 2027.

Marwa amesema katika mwaka wa fedha 2026/27, TTCL inalenga kujenga maungio mengine 400,000 kwa kutumia teknolojia ya GPON, inayowezesha kuwafikia wateja wengi zaidi kwa wakati mmoja.