September 15, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mradi wa Mawasiliano waongeza ufanisi huduma za Serikali

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Dar

MRADI wa Mawasiliano umewezesha kuboresha upatikanaji wa mawasiliano na huduma za Serikali kwa njia ya kielektroniki hususani maeneo ya vijijini.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa TEHAMA Ofisi ya Rais Manajimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Priscus Kiwango jijini Dar-es-Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Kiwango amesema,mradi huo umeunganisha ofisi za Serikali ikiwemo Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuwezesha matumizi ya mifumo kama PEPMIS kwa ajili ya kupima utendaji wa watumishi wa umma.

Amesema,Daftari la Huduma za Serikali linamwezesha mwananchi kupata taarifa muhimu kuhusu huduma ikiwemo mahali inapotolewa,mahitaji,muda na gharama hivyo kupunguza usumbufu katika kuzifuata.

Pia amesema,mradi huo umewezesha kuunganisha mifumo mbalimbali ya Serikali ili iweze kubadilishana taarifa na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma.