September 12, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenyekiti Act Wazalendo Dodoma ahaidi siasa za hoja

Na Mwandishi wetu,TimesMajira Online,Chamwino.

VIONGOZI wa ACT Wazalendo ngazi ya Mkoa wa Dodoma wamefanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma kukutana na Mkuu wa Wilaya ya Chamwino,Janeth Mayanja,Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chamwino, na Mkuu wa kituo cha polisi Wilaya ya Chamwino.

Viongozi wa ACT Wazalendo Mkoa wa Dodoma waliofanya ziara katika wilaya hiyo ni Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Mkoa wa Dodoma,Rev David Majanjara na Katibu wa ACT Wazalendo Mkoa wa Dodoma Sunday Madinda.

Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Mkoa wa Dodoma Rev,David Majanjala,akizungumza na viongozi wa Halmashauri ya Chamwino amesema lengo kubwa ni kuhakikisha wanafanya kazi za siasa katika halmashauri hiyo kwa kujenga hoja na si ugomvi wala chuki kati ya viongozi wa Serikali na vyama vya siasa.

Rev.Majanjara amesema kuwa nia ya vyama vya siasa hususani wa mlengo wa kushoto ni kuhakikisha wanawatetea wananchi na kubishana na Serikali kwa hoja na si kwa kutumia kauli za dharau na matusi.

Mwenyekiti huyo amelazimika kutoa maelezo hayo baada ya kujitokeza mmoja wa mtu aliyejinadi kuwa ni kiongozi na wanachama wa chama hicho kutumia nembo ya chama kuwadhalilisha viongozi wa Serikali na ndani ya chama jambo ambalo si la kiungwana.

Rev Majanjala alisema kuwa uongozi wa ACT Wazalendo Mkoa wa Dodoma hupo tayari kufanya kazi na viongozi wa Serikali ili kutengeneza ufanisi wa pamoja kwa manufaa ya wananchi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Janeth Mayanja alisema kuwa Serikali wapo tayari kufanya kazi na viongozi wote wa kisiasa ili mradi kila mmoja atimize wajibu wake.

“Tunajua kabisa kuwa vyama vyote vya siasa vipo kwa ajili ya kusimamia maendeleo na sisi viongozi wa Serikali tupo kwa ajili ya kutimiza malengo na mipango ya serikali kwa nia ya maendeleo ya wananchi.

“Najua tukishirikiana kwa umoja tutasimama pamoja kwa nia ya kuwapatia maendeleo wananchi na tukipishana tutapelekea wananchi kuchelewa kimaendeleo”akieleza Mkuu wa Wilaya Janeth.