Na Mwandishi Wetu.TimesMajira
MAKAMU wa Rais, Deogratius Ndejembi ameagiza mamlaka na tasisi zinazohusika kuchukua hatua za haraka kujiandaa ili kuzuia na kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño zinazotarajiwa kuanza Oktoba, 2026.
Makamu wa Rais ametoa maagizo hayo, mara baada ya kupokea taarifa ya utayari na maandalizi ya Serikali kufuatia tahadhari iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kuhusu mvua za El- nino, katika kikao kilichofanyika Ofisi ya Makamu wa Rais Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na viongozi pamoja na timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Wizara ya Ujenzi pamoja na Taasisi zilizochini ya Wizara hizo, Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa taasisi zote zinazohusika, kufanya kazi kwa pamoja na kuchukua hatua za tahadhari mapema ili kuzuia au kupunguza athari zinazoweza kutokea kwa wananchi kufuatia ujio wa mvua hizo.

Pia amesisitiza umuhimu wa vyombo vya ulinzi na usalama kushirikishwa katika maandalizi hayo ili kuwa na nguvu kazi ya kutosha pamoja na kuimarisha uwezo wa Serikali wa kuzuia, kupunguza na kukabiliana kwa haraka na athari zinazoweza kujitokeza.
“Ifanyike kampeni ya haraka, mikondo na mifereji ya maji izibuliwe, na barabara ziandaliwe,” amesisitiza Makamu wa Rais. Ameelekeza taka, tope na udongo unaotolewa baada ya kuzibua mitaro na mifereji katika maeneo mbalimbali kuondolewa mara moja na kutupwa katika maeneo yaliyotengwa, badala ya kuachwa kandokando ya barabara ambako unaweza kurejea kwenye mifereji wakati mvua zinapoanza.

Makamu wa Rais pia ameagiza mamlaka husika kuwasimamia wakandarasi wanaotekeleza miradi ya ujenzi wa barabara, kuchukua hatua za haraka kusambaza vifusi vilivyorundikwa katika maeneo yenye shughuli za ujenzi, akisisitiza kuwa kazi hiyo haipaswi kusubiri hadi mvua zianze kunyesha kwani husababisha usumbufu na kero kwa wananchi.

More Stories
Mpanju atoa wito wadau kuimarisha Mabaraza ya watoto
Wasusi wataka programu ya Darling ipanuke
TCRA,Wadau Rukwa wakutana kujadili uhalifu mtandaoni