Na Penina Malundo,TimesMajira
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imekamata shehena ya dawa na vifaa tiba visivyosajiliwa yenye thamani ya takribani Sh milioni 360 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Terminal 3.
Hatua hiyo ni sehemu ya operesheni zinazoendelea za TMDA kudhibiti uingizaji na usambazaji wa bidhaa tiba kinyume cha sheria, kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo, amesema shehena hiyo ilikamatwa katika matukio mbalimbali, likiwemo la Septemba 7, 2026 ambapo masanduku 20 yenye dawa zisizosajiliwa yenye thamani ya Sh milioni 310 yalikamatwa.
Amesema pia Septemba 9, 2026, TMDA ilikamata shehena nyingine ya dawa za sindano aina ya Lignocaine, Bupivacaine, Adrenaline na vitamini, pamoja na Ozempic (semaglutide), GLP-1 na vifaa tiba vya meno bandia.
Dkt. Fimbo amesema bidhaa hizo ni hatari kwa afya ya wananchi kwa kuwa ubora, usalama na ufanisi wake haujathibitishwa na TMDA, hivyo matumizi yake yanaweza kusababisha madhara ikiwemo kuchelewa kupona, usugu wa dawa, ulemavu na hata kifo.
Amesema baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakitumia njia mbalimbali kuingiza bidhaa hizo nchini, ikiwemo kuzificha kwenye masanduku na vifurushi vinavyosafirishwa kwa ndege na mabasi.

Kwa mujibu wa Dkt. Fimbo, TMDA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi inaendelea na uchunguzi ili kuwabaini na kuwakamata wahusika pamoja na mtandao unaojihusisha na biashara hiyo haramu.
Amesema mamlaka hiyo imeimarisha mifumo ya ukaguzi kwa kuunganisha mifumo yake na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), hatua inayosaidia kubaini mapema nyaraka bandia na shehena zisizo na vibali.
Pia imeongeza ukaguzi wa kushtukiza katika mipaka, viwanja vya ndege na bandari, huku ikiendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwemo Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).

Dkt. Fimbo amewakumbusha wafanyabiashara wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi kuzingatia Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba, Sura ya 219, akisisitiza kuwa ni marufuku kuingiza bidhaa hizo nchini bila kibali cha TMDA.

More Stories
Rashal yaharakisha Ujenzi wa Bomba la Gesi Kisemvule Mbagala
Matatani kwa kumuua mkewe,kisa wivu wa mapenzi
NMB yapanua malipo ya Kidijitali Kariakoo Festival