September 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vyama vya Siasa vyatakiwa kuwa Mabalozi wa Bima



VYAMA vya siasa nchini vimetakiwa kutumia majukwaa yao kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote, kwa kuwa afya ni haki ya kila mwananchi bila kujali itikadi, umri, jinsia au nafasi yake katika jamii.


Wito huo umetolewa Visiwani Zanzibar na Kaimu Waziri wa Afya, Dkt. Saada Mkuya Salum, ambaye pia ni Mbunge wa Welezo, wakati wa semina iliyowakutanisha wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa na wataalamu kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu Bima ya Afya kwa Wote.


Dkt. Mkuya amesema wanasiasa wana mtandao mpana wa kuwafikia wananchi kuanzia ngazi ya jamii hadi taifa, hivyo wana nafasi muhimu ya kuwa mabalozi wa elimu kuhusu afya na bima ya afya.


Amesema ushiriki wa vyama vya siasa katika kutoa elimu hiyo unaweza kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kuwa na bima ya afya na namna inavyoweza kusaidia kulinda afya na ustawi wa familia.


“Bima ya afya inalinda mwananchi na familia dhidi ya gharama kubwa za matibabu. Hili si suala la chama cha siasa, bali ni suala la maisha na ustawi wa wananchi,” amesema Dkt. Mkuya.


Ameongeza kuwa wanasiasa wanapokutana na wananchi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo mikutano ya hadhara na majukwaa mengine, wanaweza kutumia fursa hizo kutoa elimu sahihi kuhusu umuhimu wa bima ya afya.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ally Khatib, amesema elimu iliyotolewa katika semina hiyo itawafikia viongozi wa vyama vya siasa kuanzia ngazi ya taifa, mikoa, wilaya na kata, pamoja na wanachama wao.


Amesema viongozi hao watakuwa na jukumu la kuifikisha elimu hiyo kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini, kwa lengo la kuongeza uelewa na ushiriki katika mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.


“Tunachojifunza hapa hakitaishia kwa wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa. Tutakwenda kuwaelimisha viongozi wetu wa kitaifa, mikoa, wilaya, kata na wanachama, ambao nao wataifikisha elimu hii kwa wananchi,” amesema Khatib.


Naye Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Mohamed Ahmed, amesema semina hiyo inalenga kuwawezesha viongozi na wawakilishi wa vyama vya siasa kupata uelewa sahihi kuhusu mifumo ya bima ya afya nchini, ili waweze kutoa elimu sahihi kwa wananchi.


Amesema uelewa wa viongozi wa kisiasa ni muhimu kwa kuwa wana nafasi kubwa ya kuhamasisha wananchi kushiriki katika mipango mbalimbali ya Serikali inayolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za afya.


Akizungumza katika semina hiyo, Dkt. David Mwanesano kutoka NHIF amesema Serikali imeanza kutekeleza mpango wa Bima ya Afya kwa Wote kwa awamu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha wananchi wanapata kinga dhidi ya changamoto za gharama za matibabu.


Amesema hadi sasa jumla ya kaya 276,400 zimekwishaandikishwa katika mpango huo na kuanza kupata huduma za afya.


Amesisitiza kuwa ushirikiano wa wadau mbalimbali, wakiwemo viongozi wa kisiasa, ni muhimu katika kufanikisha azma ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma za matibabu bila kukabiliwa na mzigo mkubwa wa gharama za matibabu.