
Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOnline,Mbeya
Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya wamejitolea kuunga mkono sekta ya elimu kwa kuchanga fedha na kununua mashine kubwa ya kisasa ya kudurufu nyaraka (photocopy) kwa ajili ya Shule ya Sekondari Sinde mkoani Mbeya.
Msaada huo unalenga kutatua changamoto iliyokuwa inawakabili wanafunzi na walimu wa shule hiyo, hususan katika uandaaji na udurufu wa mitihani pamoja na nyaraka nyingine muhimu za kielimu.
Awali, shule hiyo ilikabiliwa na changamoto ya hitilafu ya mashine iliyokuwa ikitumika, hali iliyowalazimu wanafunzi na walimu wakati mwingine kutafuta huduma za kudurufu nyaraka nje ya eneo la shule. Hali hiyo ilikuwa ikisababisha ucheleweshaji na kuathiri ufanisi wa shughuli za kitaaluma.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mashine hiyo September 7,2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, Dkt. Godlove Mbwanji, amesema watumishi wa hospitali hiyo wameona umuhimu wa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha elimu, kwa kuanzia katika ngazi za msingi ambako wataalamu wa baadaye huandaliwa.
“Sisi kama taasisi ya afya tunapokea watu ambao tayari wamekuwa wataalamu, wakiwemo wauguzi, madaktari na wataalamu wa fani nyingine. Tuliona ni vyema nasi tukatoa mchango wetu katika maeneo ambako wataalamu hao wanakuzwa na kuandaliwa, ikiwemo shule hii,” amesema Dkt. Mbwanji.
Amesema Serikali inaendelea kufanya kazi kubwa katika kuboresha sekta ya elimu, lakini kutokana na mahitaji yaliyopo, ushirikiano wa taasisi mbalimbali na wananchi ni muhimu katika kuchangia maendeleo ya taifa.

Dkt. Mbwanji ameongeza kuwa kuwawezesha wanafunzi kupata mazingira bora ya kujifunzia ni sehemu ya kuandaa tegemeo la taifa la kesho, kwani miongoni mwa wanafunzi hao watapatikana madaktari, wauguzi na wataalamu wengine watakaolitumikia taifa siku zijazo.
Kwa upande wao, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa hospitali hiyo, Bi. Myriam Msalale, pamoja na Afisa Rasilimali Watu, Jacqueline, wamesema msaada huo ni kielelezo cha imani ya watumishi wa hospitali katika umuhimu wa elimu kwa maendeleo ya taifa.
Wamesema kazi na mitihani itakayokuwa ikidurufiwa kwa kutumia mashine hiyo zitasaidia kurahisisha mchakato wa ujifunzaji na ufundishaji, hatua ambayo inaweza kuchangia kuongeza uelewa na kiwango cha ufaulu wa wanafunzi.
Akizungumza kwa niaba ya jumuiya ya shule hiyo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Sinde, Bi. Anatalia Valence Luwungo, amewashukuru watumishi na uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya kwa msaada huo.
Amesema shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 1,196 ilikuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa kutokana na kutokuwa na mashine ya kudurufu nyaraka, hivyo ujio wa mashine hiyo ya kisasa ni ukombozi mkubwa kwa walimu na wanafunzi.
Nao wawakilishi wa wanafunzi wa shule hiyo, Noel Sanga na Vanesa Kyando, walitoa shukrani zao kwa watumishi wa hospitali hiyo na kueleza kuwa msaada huo utakuwa chachu ya kuongeza bidii katika masomo yao.
Wamesema upatikanaji wa mashine hiyo utarahisisha shughuli za kitaaluma na kuwapa fursa nzuri zaidi ya kujiandaa kwa ajili ya mitihani, huku wakiahidi kuongeza juhudi ili kupata matokeo bora.

More Stories
Wasusi Gongolamboto wanufaika na loyalty program
TANESCO yatunukiwa Tuzo kutambua mchango wake
wanawake magereza wahimizwa kujenga uwezo , kutumia fursa kidijitali