September 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ajenda ya Msichana 2026 kuinua sauti za wasichana

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

MASHIRIKA yanayotetea na kukuza haki za wasichana kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, yameandaa Jukwaa la Ajenda ya Msichana 2026, litakalowakutanisha wasichana kutoka mikoa mbalimbali nchini kujadili changamoto, mawazo na mapendekezo yao kuhusu maendeleo ya taifa.

Jukwaa hilo litakuwa la tisa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2017 na litabeba kaulimbiu “Kuinua Sauti za Wasichana kwa Maendeleo Endelevu.”

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kijitonyama Science, Najma Likunda, amesema jukwaa hilo linalenga kuwapa wasichana nafasi ya kueleza changamoto zao moja kwa moja kwa taasisi, wadau wa maendeleo na watoa maamuzi.

Amesema washiriki wanatarajiwa kutoka Dar es Salaam, Pwani, Arusha, Kilimanjaro, Morogoro, Mwanza, Dodoma na Tabora.

Kwa upande wake, Mwanafunzi mwenzake wa Shule ya Makongo Juu, Jenifa Toji, amesema kwa miaka tisa jukwaa hilo limewafikia wasichana na wanawake vijana zaidi ya 15,000, likiwapa nafasi ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kushiriki katika utetezi wa haki zao.

“Mwaka huu, mjadala utaelekezwa zaidi katika kuhakikisha sauti za wasichana zinasikika na kuchukuliwa hatua, badala ya kuishia katika kuwashirikisha kwenye matukio,”amesema.

Naye mwakilishi wa Wote Sawa, Miriam Mtagulwa, amesema jukwaa hilo litajadili masuala yanayogusa maisha ya wasichana, yakiwemo elimu, usawa wa kijinsia, usalama, teknolojia, uongozi na fursa za kiuchumi.

Amesema changamoto za mimba na ndoa za utotoni, kuacha shule, umaskini, ukatili pamoja na ukosefu wa fursa za kidijitali ni miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa.

Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wasichana kutoka Msichana Initiative, Letisia Mswaki, amesema teknolojia pia itapewa kipaumbele kutokana na nafasi yake katika kuwawezesha wasichana kupata elimu, taarifa, ajira, biashara na kushiriki katika shughuli za kijamii na kiuchumi.

Ameonya kuwa kasi ya mabadiliko ya kidijitali inaweza kuongeza pengo la kijinsia iwapo wasichana hawatapewa fursa sawa ya kupata vifaa, intaneti na ujuzi wa kidijitali.

Kwa mujibu wa Verynice Kirumu kutoka GLAMI, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima.