Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
SERIKALI imewataka wadau wa maendeleo nchini, wakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali, kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuwawezesha watoto wa kike kushiriki kikamilifu katika masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu.
Kauli hiyo ilitolewa juzi jijini Dar es Salaam na Mwakilishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Felister Mapunda, wakati wa uzinduzi wa mfumo wa kidijitali wa One Girl Plus unaotekelezwa na Msichana Initiative.
Amesema Serikali kupitia Sera ya Elimu na Mafunzo pamoja na mtaala ulioboreshwa, imeendelea kusisitiza matumizi ya sayansi na teknolojia katika elimu ili kuwaandaa vijana kukabiliana na mahitaji ya sasa ya jamii na soko la ajira.
“Unapomuelimisha msichana haumsaidii peke yake, unawezesha familia, unaimarisha jamii na unawekeza katika kizazi kijacho,” amesema.
Mapunda amesema msichana mwenye ujuzi ana uwezo wa kufanya maamuzi sahihi, kujilinda, kujiamini, kujenga maisha yake na kuwa chachu ya mabadiliko katika jamii.
Amesema mfumo wa One Girl Plus unaweza kuwa daraja kati ya msichana na fursa, kati ya ndoto na utekelezaji, pamoja na kati ya changamoto za leo na Tanzania inayotarajiwa kesho.

Aidha, amesema Wizara ya Elimu imekuwa ikishirikiana na Msichana Initiative katika kuhakikisha wasichana wanapata haki ya elimu na mazingira yanayowawezesha kuishi kwa heshima na kufikia ndoto zao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Msichana Initiative, Consolata Chikoti, amesema pamoja na wasichana kupata elimu shuleni, bado kuna umuhimu wa kuwajengea stadi za maisha zinazowasaidia kujitambua, kujiamini na kuweka malengo.
Amesema hali hiyo imeifanya taasisi hiyo kutumia teknolojia kama njia ya kuwafikia wasichana wengi zaidi.
“Tumeona kwamba ijapokuwa wasichana wanapata elimu mashuleni, kuna pengo kubwa katika kupata stadi za maisha zinazowafundisha kujitambua, kujiamini na kujiwekea malengo,” amesema.
Chikoti amesema One Girl Plus imejengwa ili kuwasaidia wasichana kukuza kujiamini, kupata stadi za maisha na kuwa na uwezo wa kuweka malengo ya maisha yao.
Naye Mwakilishi, Karimjee Foundation,Caren Rowland ameipongeza Shirika la msichana kuzindua Programu hiyo na kusema kuwa Karimjee Foundation imeendelea kushirikiana na shirika hilo katika juhudi nyingine zinazolenga kuondoa vikwazo vinavyowakabili wasichana katika kupata elimu, ikiwemo One Girl One Bike, mpango unaosaidia kukabiliana na changamoto ya umbali wa kwenda na kurudi shuleni kwa kuwapatia wasichana baiskeli.
“Tunaamini kuwa kila msichana anapaswa kuwa na fursa ya kujifunza na kufikia uwezo wake bila kuzuiwa na umbali au mazingira anayotoka.
“Ushirikiano wetu na Msichana Initiative, kuanzia One Girl One Bike hadi hatua hii ya One Girl Plus Digital Platform, unaakisi dhamira ya kuwekeza katika suluhisho zinazowafikia wasichana walipo, tunaweza kuwasaidia wasichana wengi zaidi kujifunza,kujenga,kujiamini, kuweka malengo na kuandaa mustakabali Bora zaidi kwa maendeleo ya wasichana,”amesema
Aidha amesema kupitia ushirikiano wa aina hii, Msichana Initiative na Karimjee Foundation unaonesha namna wadau mbalimbali wanavyoweza kushirikiana kuleta suluhisho zinazogusa changamoto halisi zinazowakabili wasichana kuanzia namna wanavyofika shuleni hadi namna wanavyoweza kupata maarifa kupitia teknolojia.

Naye Mkuu wa Mawasiliano wa Msichana Initiative, Sara Bedah, amesema programu hiyo ilianza miaka minne iliyopita kwa kutumia mikutano ya ana kwa ana shuleni na hadi sasa imewafikia zaidi ya wasichana 10,000.
Amesema kuanzishwa kwa mfumo wa kidijitali kutasaidia kuongeza wigo wa programu hiyo na kuwafikia wasichana wengi zaidi katika maeneo mbalimbali.

More Stories
Serikali yaridhishwa maandalizi NHIF kuelekea AFCON
Samizi ataka NHIF kuongeza kasi usajili wanachama
EACOP kukamilika Januari 2027