September 5, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samizi ataka NHIF kuongeza kasi usajili wanachama



NAIBU Waziri wa Afya, Dkt. Florence George Samizi, ameipongeza Bodi ya Wafanyakazi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kuwa miongoni mwa mabaraza bora nchini, huku akitaka mfuko huo kuongeza kasi ya usajili wa wanachama kwa kutumia mifumo ya kidijitali ili kufikia lengo la Bima ya Afya kwa Wote.


Dkt. Samizi amesema amefurahishwa na ongezeko la uandikishaji wa wanachama wa NHIF, ambapo katika mwaka wa fedha 2025/2026 mfuko umefikia asilimia 10.7 ya wananchi, kutoka asilimia nane iliyodumu kwa takribani miaka 10.


Amesema ongezeko hilo ni hatua nzuri, lakini NHIF inapaswa kuongeza kasi zaidi kwa kutumia TEHAMA katika usajili wa wananchi ili kutekeleza ahadi ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za bima ya afya.


“Matumizi ya TEHAMA katika usajili yatawezesha kuwafikia wananchi wengi zaidi na kusaidia kutimiza azma ya Serikali ya kuwa na Bima ya Afya kwa Wote. Hii itasaidia wananchi kujikinga na athari za umaskini zinazoweza kusababishwa na gharama za matibabu,” amesema.


Dkt. Samizi ametoa kauli hiyo wakati wa Mkutano wa Nne wa Baraza la Nne la Wafanyakazi wa NHIF uliofanyika jijini Arusha.


Aidha, ameitaka menejimenti na watumishi wa NHIF kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia uadilifu, weledi na uwajibikaji, huku wakihakikisha kero za wananchi zinasikilizwa na kutatuliwa kwa wakati.


Amesisitiza pia umuhimu wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu faida na umuhimu wa kuwa na bima ya afya, pamoja na kuboresha huduma na kuweka mifumo madhubuti ya kupokea na kufanyia kazi mrejesho kutoka kwa wananchi.


Katika kuelekea maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa NHIF, Dkt. Samizi amesema ni muhimu mfuko huo kuonesha mafanikio yaliyopatikana na kueleza mchango wake katika kuboresha huduma za afya nchini.


Amesema uwepo wa NHIF umechangia kuboresha huduma za afya kupitia ulipaji wa madai na utoaji wa mikopo kwa vituo vya kutolea huduma za afya.


“Mlianza na vituo vichache sana mwaka 2001, lakini sasa katika mwaka wa fedha 2025/2026 mmefikia zaidi ya vituo 10,600 vilivyosajiliwa nchini. Ni muhimu kuwaonesha wananchi hatua kubwa iliyofikiwa,” amesema.


Amesema NHIF inapaswa pia kueleza namna ilivyokabiliana na changamoto mbalimbali tangu kuanzishwa kwake na hatua zilizochukuliwa ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.


Kwa mujibu wa Dkt. Samizi, mafanikio hayo yamechangiwa na kujituma, ushirikiano, umoja na mshikamano miongoni mwa watumishi wa NHIF katika kutekeleza malengo ya mfuko na jitihada za Serikali za kuhakikisha wananchi wanapata huduma za bima ya afya.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dkt. Irene Isaka, amesema mfuko umeendelea kupata mafanikio mbalimbali, ikiwemo kupunguza muda wa kulipa madai kutoka zaidi ya siku 90 hadi wastani wa siku 50 katika mwaka wa fedha 2025/2026.


Amesema pia ziada ya mfuko imeongezeka kwa asilimia 57, matumizi yamepungua kwa asilimia 13, huku uwekezaji ukiongezeka kwa asilimia 106.

Ameeleza kuwa mafanikio hayo yamewezesha NHIF kuendelea na kifurushi cha wanafunzi cha Toto Afya, pamoja na kusajili vifurushi vya Tarangire, Mikumi, Ngorongoro, Serengeti, Tanzanite na Umoja Afya kwa ajili ya vikundi, ambacho kinagharimu Shilingi 60,000 kwa matibabu ya mwaka mzima.


Dkt. Isaka amesema NHIF inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kufikia malengo yake, ikiwemo matumizi ya TEHAMA katika usajili wa wanachama, uchakataji wa madai na kupambana na udanganyifu.


Amesema mfuko pia unaendelea kushirikisha sekta binafsi katika usajili wa wanachama na utoaji wa huduma za matibabu.


Kwa upande wake, mwakilishi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE), Paul, amepongeza Baraza la Wafanyakazi la NHIF kwa kuzingatia misingi ya kazi stahiki na maslahi ya wafanyakazi katika taasisi hiyo.


Baadhi ya wafanyakazi walioshiriki semina elekezi ya siku mbili wamesema wamepata maarifa na mwelekeo mpya utakaowasaidia kuboresha utendaji wao wa kazi na utoaji wa huduma kwa wananchi.