Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Bukoba
IMEELEZWA kuwa mradi wa ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP)kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga hapa nchini,utekelezaji wake umefikia asilimia 87.7 na unatarajia kukamilika na kuanza rasmi Januari 15,2027,ambapo bomba hilo litakuwa na uwezo wa kusafirisha mapipa takribani 200,000 ya mafuta kwa siku.
Mradi huo ambao ulisainiwa mkataba wake mwaka 2021 utadumu takribani miaka 25.
Mratibu wa utekelezaji wa mradi wa huo,Jumanne Saidi amezungumza hayo wakati akitoa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari mkoani Kagera juu ya mradi wa bomba la mafuta na maendeleo yake.

Ambapo amesema kiasi cha sh.bilioni 35.6 zimetumika kulipa fidia kwa wananchi wapatao 10,144 maeneo yote yanayopitiwa na mradi huo huku
nyumba zilizoguswa ni 340,kati ya hizo kwa Mkoa wa Kagera ni nyumba 119 ambapo eneo la ardhi lililotwaliwa kwenye mradi huo ni ekari 1395.2 za mkoa huo.
“Mikoa inayopitiwa na bomba la mafuta ni nane ambayo ni Kagera,Geita, Shinyanga,Tabora,Singida,Manyara, Dodoma na Tanga.Kwa Mkoa wa Kagera unapita katika wilaya nne za Misenyi, Bukoba vijijini, Muleba na Biharamlo,” amesema Saidi.
Saidi amesema,mradi utakapoanza Tanzania itanufaika kwani italipwa dola 12.77 kwa kila pipa na yanatarajiwa kuvunwa mapipa 216,000 kwa siku moja
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Marie Nsellemu amesema,Mkoa wa Kagera ni wa kwanza kwa kupitiwa na bomba la mafuta katika wilaya nne.
Nsellemu amesema,kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga mradi unakatiza kilomita 1,480 hivyo amewataka wananchi kulinda miradi inayofanywa na Serikali kupitia TPDC.
Akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Kagera Isaya Tendega amesema, tangu mchakato mzima wa utafiti wa kimazingira ulipoanza kufanyika mpaka sasa mradi unaelekea mwisho mkoa huo umenufaika kwa sehemu kubwa kiuchumi.
“Ajira za moja kwa moja zimepatikana katika maeneo mradi unapopitia pia kwa vijana,mama ntilie na wafanyabiashara.Pia kumekuwa na hatua mbalimbali mfano hatua za utoaji wa ardhi ambapo sheria za kimataifa zimezingatiwa ili kuhakikisha kwamba mwananchi anapoondolewa kwenye eneo lake kupisha mradi basi anajengewa mazingira mazuri zaidi ya yale aliyokuwa nayo,”amesema Tendega.

Ameeleza kuwa,hilo limedhibitika kwani wapo waliokubali kujengewa nyumba bora zaidi na wapo waliopewa fedha taslimu kwenda kujenga wanapotaka wao.
Amesema hata waliojengewa nyumba pia walipata kiasi cha fedha hivyo wananchi wote waliopitiwa na mradi wamenufaika.


More Stories
Wananzengo wamkataa Kayala mbele ya Polisi,nyumba yake yanusurika kuchomwa moto
TMA yatakiwa kuimarisha utabiri wa hali ya hewa
Haule aungana na wananchi kuchimba msingi wa shule