Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Mwanza
MHITIMU wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Gladness Silayo,amegeuza elimu ya Shahada ya Uhasibu na Fedha kuwa fursa ya ujasiriamali kwa kuanzisha kiwanda cha kutengeneza viatu cha Pacha Shoes Company, kwa kutumia ngozi inayopatikana hapa nchini.
Silayo aliyehitimu mwaka 2023,alianza biashara hiyo mwaka 2023 ambapo wazo la kuanzisha kiwanda, alilipata Septemba,2023, alipokwenda kufunga ndoa na mumewe, ili kukabiliana na changamoto ya kupata ajira na kwa sasa ameajiri wafanyakazi kadhaa.

Bidhaa zinazozalishwa na kiwanda hicho zimekuwa kivutio katika Maonesho ya 21 ya Biashara ya Afrika Mashariki (MEATF 2026), yanayofanyika katika Uwanja wa Furahisha wilayani Ilemela mkoani Mwanza.
Ambapo Silayo amesema,wazo la kuanzisha uzalishaji wa viatu lilitokana na utafiti alioufanya kuhusu mahitaji ya soko, ambapo alibaini kuwa kuna mahitaji ya viatu vyenye ukubwa maalumu na ubora unaodumu.
Akizungumza jana wakati wa maonesho hayo, Silayo amesema,baada ya kushindwa kupata ajira aliamua kutumia maarifa aliyoyapata chuoni kuanzisha biashara ya uzalishaji wa viatu, akiamini kuwa ujasiriamali ungekuwa njia ya kujiajiri na kutoa ajira kwa wengine.
“Elimu ya ujasiriamali niliyopata imenisaidia.Namshukuru Dkt.Laurent Sunda, alikuwa akitufundisha somo la ujasiriamali na kutushauri vijana kuwa wabunifu.Nikiwa chuoni nilianza kutengeneza bidhaa ya mafuta ya kupaka, hatua iliyonisaidia kujenga ujuzi wa vitendo na kuniandaa kwa shughuli za uzalishaji baada ya kuhitimu,”amesema Silayo.
“Tangu nianze uzalishaji nimekuwa nikifanya utafiti na kuboresha bidhaa zangu ikiwemo kutafuta malighafi na teknolojia zinazoweza kuongeza uimara wa viatu.Nimeboresha bidhaa yangu, natumia gundi ya moto ambayo ni gharama kubwa, tunaichanganya na gundi aina nyingine inasababisha viatu visibanduke,”amesema.
Hata hivyo amesema,pamoja na mwitikio mzuri wa wananchi kwa bidhaa hizo, changamoto kubwa inayomkabili ni upatikanaji wa soko kutokana na gharama za uzalishaji kuwa kubwa ikilinganishwa na bidhaa nyingine zinazouzwa kwa bei ya chini.
Amesema hali hiyo inafanya baadhi ya wateja kuangalia zaidi bei kuliko ubora wa bidhaa, jambo linaloweka changamoto kwa wazalishaji wanaotumia malighafi bora za ndani na kuzingatia ubora katika uzalishaji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Utawala wa IFM Kampasi ya Mwanza,Dkt.Laurent Joseph, akizungumzia ubunifu uliofanywa na mhitimu wa chuo hicho kwa kutumia malighafi za ndani amesema, ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuchangia katika kutatua changamoto ya ajira na kukuza uchumi.
Dkt.Joseph amesema,matumizi ya malighafi za ndani yanaweza kupunguza utegemezi wa malighafi zinazoagizwa kutoka nje ya nchi, huku yakitoa nafasi kwa Watanzania kuongeza thamani ya rasilimali zinazopatikana nchini.
Naye Mhadhiri Msaidizi na Mkuu wa Taaluma wa IFM Kampasi ya Mwanza, Bahati Maneno amesema,mafanikio ya wahitimu kama Silayo yanaonesha umuhimu wa elimu ya juu katika kuwawezesha vijana kutumia maarifa yao kuanzisha shughuli za uzalishaji na kutoa ajira kwa wengine.
Maneno amesema,bidhaa za ubunifu zinazotumia malighafi za ndani, zikiwemo viatu vya ngozi vya Silayo, zinatumika kuonesha uwezo wa vijana katika kuongeza thamani ya malighafi na kuzalisha bidhaa zinazoweza kushindana sokoni.


More Stories
TanTrade yafungua soko Afrika Mashariki
REA yatoa pole kifo cha Mfalme Harald V
Miss Universe Tanzania, Hexagon zaingia ubia