September 2, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DCEA yazindua klabu kupinga dawa za kulevya vyuoni

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), imezindua klabu za kupiga vita dawa za kulevya katika vyuo na vyuo vikuu kote nchini.

Lengo likiwa, ni sehemu ya jitihada za kuimarisha mapambano dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya miongoni mwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Uzinduzi huo umelenga kuimarisha kinga, kuongeza uelewa na kujenga mazingira yatakayowawezesha vijana kufanya maamuzi salama na yenye tija kwa mustakabali wa maisha yao na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa klabu hizo, uliofanyika Septemba 1, 2026 katika Ukumbi wa Maktaba Mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema klabu hizo zitatumika pia kutafakari tatizo la dawa za kulevya kwa mtazamo wa kitaaluma.

Amesema, uraibu wa dawa za kulevya ni tatizo linalopoteza utu na kusababisha mateso kwa vijana, hivyo kukabiliana nalo kunahitaji majibu ya kina na hatua za uzuiaji zinazohusisha jamii kikamilifu.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema tatizo la dawa za kulevya lina athari katika afya ya jamii, usalama, uchumi, familia na maendeleo ya Taifa, hivyo Serikali imeweka mikakati ya kupunguza upatikanaji na uhitaji wa dawa hizo, kupunguza madhara yatokanayo na matumizi pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kitaifa, kikanda na kimataifa.

Amesema, mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa kupunguza uhitaji wa dawa za kulevya, unaosisitiza kinga kupitia elimu, uhamasishaji na hatua za kuzuia watu kuanza kutumia dawa hizo.

Aidha, amesema wanafunzi wa vyuo vikuu ni miongoni mwa makundi muhimu yanayolengwa katika utoaji wa elimu hiyo.

Amesema, baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu wameshindwa kuendelea na masomo kutokana na ushawishi wa makundi rika na kujihusisha na starehe pamoja na matumizi ya dawa za kulevya. Huku akisema vyuo vikuu ni vituo vya kuzalisha wataalamu na maarifa, hivyo wanafunzi wanapaswa kushirikishwa katika tafiti zinazohusu sababu, vihatarishi, mwenendo na madhara ya tatizo hilo.

Hata hivyo amesema, tafiti hizo zitasaidia kuongeza uelewa wa taifa kuhusu dawa za kulevya na kutoa msingi wa kuboresha sera, mipango na afua za Serikali.

Amewataka wataalamu kutoka sekta mbalimbali kujikita katika tafiti, akieleza kuwa wataalamu wa afya wanaweza kuchunguza madhara na tiba, saikolojia na jamii kuchunguza vichocheo vya matumizi, huku wataalamu wa sheria na TEHAMA wakichangia katika maeneo yao.

Awali, Mwakilishi wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (Vyuo vya Kati na Vyuo Vikuu) Tanzania (TAHILISO), Aron Seni, amesema mazingira ya maisha ya chuoni yanaweza kuwaweka vijana katika hatari ya kushawishika kutumia dawa za kulevya kutokana na uhuru wa maisha, shinikizo kutoka kwa marafiki na changamoto mbalimbali za maisha.

Seni amesema, klabu hizo hazipaswi kuwa vikundi vya kufanya shughuli za kawaida au kupiga picha kwa ajili ya mitandao ya kijamii, bali zinapaswa kuwa nguzo za elimu, ulinzi na ukombozi wa vijana.

Klabu hizo zitatoa nafasi salama kwa wanafunzi wanaokabiliwa na changamoto za matumizi ya dawa za kulevya kupata elimu, ushauri na msaada bila kuhukumiwa.