Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online,Mwanza
CHUO cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Kampasi ya Mwanza, kimesema ubunifu wa bidhaa unaofanywa na wanafunzi wake kwa kutumia malighafi za ndani umevutia wananchi wanaotembelea banda la chuo hicho katika Maonesho ya 21 ya Biashara ya Afrika Mashariki (MEATF 2026).
Kauli hiyo imetolewa Septemba Mosi,2026 na Mkuu wa Utawala wa IFM, Kampasi ya Mwanza, Dkt.Laurent Joseph katika banda lao kwenye maonesho hayo yanayofanyika katika uwanja wa Furahisha wilayani Ilemela mkoani Mwanza, yakiwa na kauli mbui,”Usalama na Amani ni Kichocheo cha Biashara na Uwekezaji”.

Dkt.Joseph amesema,bidhaa hizo zimekuwa kivutio kutokana na ubunifu wa wanafunzi unaolenga kutumia malighafi zinazopatikana hapa nchini katika kutengeneza bidhaa zinazoweza kusaidia kutatua changamoto mbalimbali za jamii.
Amesema matumizi ya malighafi za ndani katika kutengeneza bidhaa yanaweza kusaidia kupunguza utegemezi wa malighafi zinazoagizwa kutoka nje ya nchi, huku yakitoa nafasi kwa ubunifu na uzalishaji wa bidhaa ndani ya nchi.
“Chuo kimejipanga kuandaa vijana wabunifu watakaosaidia kukuza sekta ya viwanda na kutatua changamoto za jamii na ajira. Hivyo, tunampongeza Dkt. Samia na Serikali anayoiongoza katika utatuzi wa changamoto za jamii,”amesema Dkt.Joseph.
Kwa upande wake Mhadhiri Msaidizi na Mkuu wa Taaluma wa IFM, Kampasi ya Mwanza,Bahati Maneno amesema,ushiriki wa chuo hicho katika MEATF 2026 umefungua fursa ya taasisi hiyo kujitangaza kwa jamii na kuwafikia wadau mbalimbali kutoka sekta ya umma na binafsi.
Amesema licha ya kuwa ni mara ya kwanza kwa IFM kushiriki MEATF kama taasisi ya umma, maonesho hayo yamekuwa na manufaa kwa chuo hicho, ikiwamo kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma na shughuli zinazofanywa na chuo hicho Kampasi ya Mwanza.
Pia amesema,maonesho hayo yamekuwa fursa kwa IFM kuwafikia watu wanaohitaji kujiunga na programu za elimu ya juu, hususani za Uzamili (Master’s) na Uzamivu (PhD), katika taaluma mbalimbali zinazotolewa na chuo hicho.

“Maonesho haya yametusaidia kibiashara hasa katika kufanya tafiti na kutoa ushauri wa biashara namna zinavyofanyika, ikiwemo kupata wanafunzi wanaohitaji kujiunga na kozi za juu pamoja na aina ya huduma tunazotoa za ushauri kwa taasisi za umma,”amesema Maneno.
Hata hivyo amesema,kupitia bidhaa za ubunifu na shughuli za ujasiriamali zinazooneshwa katika banda la IFM, chuo hicho kinapata fursa ya kuwasilisha uwezo wake katika tafiti, ubunifu na utoaji wa ushauri wa kitaalamu katika masuala ya biashara na maendeleo.

More Stories
Mkurugenzi MWAUWASA asisitiza huduma bora
Polisi wachunguza kifo cha mwanafunzi anayedaiwa kujirusha
Yas yatambulisha uzi mpya wa Zanzibar Marathon