Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
WAZALISHAJI, wafanyabiashara na wajasiriamali zaidi ya 300 kutoka Zanzibar na Tanzania Bara wanatarajiwa kushiriki Maonyesho ya Fahari ya Zanzibar 2026, yatakayofanyika Septemba 4 hadi 14, 2026 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA), Juma Burhan, amesema maonyesho hayo yanalenga kuwaunganisha wazalishaji na wafanyabiashara na fursa za masoko ndani na nje ya nchi, pamoja na kuhamasisha matumizi ya bidhaa zinazozalishwa nchini.
Amesema maonyesho hayo yatakuwa na shughuli mbalimbali zinazohusu afya, vijana, ubunifu, utalii, sanaa, elimu ya kodi, urasimishaji wa biashara na elimu ya fedha. Pia kutakuwa na kliniki ya biashara itakayowasaidia wajasiriamali kupata ufumbuzi wa changamoto zao.
Kwa upande wake, Kaimu Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Tahir Musa, amesema taasisi hiyo imeshirikiana na ZEA katika kurahisisha fursa za masoko na usafirishaji wa bidhaa kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar.

Amesema hadi Agosti 31, 2026, taasisi na wadau 46 kati ya 63 walioalikwa walikuwa wamethibitisha kushiriki.
Naye Mkuu wa Huduma za Kibenki kwa Wafanyabiashara wa Stanbic Bank, Fatma Ahmed, amesema benki hiyo imetoa Sh milioni 200 kama mdhamini mkuu wa maonyesho hayo kwa kutambua umuhimu wake katika kukuza biashara na uchumi.
Maonyesho hayo yanatarajiwa kuvutia zaidi ya wageni na wanunuzi 15,000 na yatafanyika chini ya kaulimbiu “Bidhaa Zetu Ndiyo Fahari Yetu.” Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kuyafungua rasmi Septemba 5, 2026.

More Stories
Ilemela yatakiwa kusimamia mifumo ukusanyaji mapato
Msigwa:Usikubali kumsajilia mtu laini ya simu
Rais Mwinyi azitaka nchi za NAM kuunganisha sauti