Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online-Mwanza
HALMASHAURI ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza imeanza kutekeleza mazingira wezeshi kwa watoto wenye mahitaji maalumu kwa kujenga mabweni mawili katika Shule ya Msingi Buswelu yenye kitengo cha watoto wenye mahitaji maalumu kwa ajili ya watoto wanaotoka Kata za mbali.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwanangu Development Tanzania (MWADETA), Walter Miya amesema hayo Agisti 28,2026 wakati wa mafunzo kwa walimu wanaofundisha watoto wenye mahitaji maalumu katika shule za awali na msingi yaliyofanyika Shule ya Msingi Buswelu, yenye kitengo cha watoto wenye mahitaji maalumu.

Miya amesema,hatua hiyo ni jitihada za Serikali hasa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, kwani mabweni hayo yatawasaidia watoto wanaotoka Kata za mbali ikiwemo Kayenze kukaa shuleni huku wakipata huduma ya elimu.
“Awali tulianza na Wilaya ya Nyamagana na sasa tupo Ilemela. Tumeanza kampeni hii na tunafurahi kuona Serikali imeanza kuangalia mahitaji ya watoto hawa,”amesema Miya.
Amesema pamoja na hatua hiyo, bado kuna changamoto ya kutotosheleza kwa vyumba vya madarasa kutokana na ongezeko la watoto wenye mahitaji maalumu, hivyo ameiomba Serikali kupitia halmashauri hiyo kuongeza vyumba vya madarasa na walimu ili uwiano wa walimu na wanafunzi uweze kuwa mzuri.
Pia amesema,katika utoaji wa elimu jumuishi watoto wenye na wasio na mahitaji maalumu wanahitaji madarasa yenye idadi ndogo ya wanafunzi ili mwalimu aweze kumudu kuwahudumia wote kulingana na mahitaji yao.

Kwa upande wake, Ofisa Elimu Maalumu Awali na Msingi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mwalimu Zakia Rashid amesema,halmashauri hiyo ina walimu 25 wa mahitaji maalumu wanaohudumia vitengo 10, huku ikiwa na wanafunzi 800 wenye mahitaji maalumu.
“Sasa hivi Shule ya Msingi Buswelu kitengo maalumu kina mabweni, hivyo kina uhitaji wa walimu wengi na wanafunzi waliopo hapa ni wengi,” amesema Mwl.Rashid.
Amesema miundombinu ya madarasa bado ni changamoto, lakini halmashauri hiyo inajitahidi kutumia iliyopo ipasavyo na kila mwaka inatenga fedha za ujenzi wa madarasa katika shule zenye vitengo vya wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
Pia amesema katika Shule ya Msingi Buswelu, kupitia miradi mbalimbali, vimejengwa vyumba viwili vya madarasa vya TRC huku mradi wa Boost ukiwa unaelekea kukamilika ukiwa na vyumba vitatu vya madarasa na matundu sita ya vyoo.
Sanjari na hayo Mwl.Rashid amewaomba wadau wa elimu kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha elimu ya watoto wenye mahitaji maalumu, kwa kuwa elimu ni chanzo cha maendeleo ya mtoto kitaaluma, kiafya na kiakili.
Mwalimu wa Elimu Maalumu wa Shule ya Msingi Kirumba, Michael Mwilenga, amesema,changamoto nyingine ni miundombinu kutokuwa rafiki kwa watoto wenye mahitaji maalumu hasa walemavu wa viungo pamoja na uhaba wa walimu wenye utaalamu huo.
Amesema,Shule ya Msingi Kirumba ina walimu wawili wenye utaalamu wa kufundisha watoto wenye mahitaji maalumu huku ikiwa na watoto 67.
“Wenye usonji, ulemavu wa viungo, ulemavu wa akili na wenye vichwa vikubwa wote ukiwachanganya kwenye darasa moja inakuwa ni changamoto sana,maana kila mmoja ana namna yake ya kufundishwa hivyo ukiwa weka pamoja mwingine anakuwa haelewi anao kama unapoteza tu muda hivyo kufanya changamoto katika ujifunzaji kwa watoto hao.Tukiwa na madarasa ya kutosha na watoto wakawekwa kulingana na mahitaji yao ni rahisi kwa sisi walimu kuwafundisha,”amesema Mwl.Mwilenga.



More Stories
MWADETA yawanoa walimu mahitaji maalumu
PBPA yahakikisha upatikanaji mafuta
NMB Bunge bonanza kuhamasisha afya na tija kazini