August 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kahama yatenga sh. bilioni 1.9 kwa zabuni za makundi maalum

Na Mwandishi wetu

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kahama imetenga bajeti ya ununuzi ya shilingi bilioni 1.9 kwa ajili ya makundi ya vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa matakwa ya Sheria ya Ununuzi wa Umma inayozitaka taasisi za umma kutenga asilimia 30 ya bajeti zao za ununuzi kwa ajili ya makundi hayo.

Akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa sheria hiyo na maelekezo ya Serikali katika Manispaa ya Kahama, Agosti 21, 2026, Afisa Maendeleo wa Manispaa hiyo, Bw. Fabiano Abisai, alimweleza Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndugu Wazo Mwang’onda, kuwa bajeti hiyo itatolewa kwa makundi yatakayopata zabuni kupitia Mfumo wa NeST.

Amesema Manispaa hiyo imesajili jumla ya makundi 326 katika Mfumo wa NeST, ambayo yako tayari kuomba zabuni za umma. Hadi sasa, makundi mawili yamepata zabuni zenye thamani ya shilingi milioni 242.45 (Sh. 242,450,000).

“Kati ya makundi yaliyosajiliwa, 173 ni ya vijana, 150 ni ya wanawake, mawili ni ya watu wenye ulemavu na moja ni la wazee. Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Halmashauri ya Manispaa ya Kahama inaendelea kuwahamasisha wananchi kuunda vikundi na kuchangamkia fursa za zabuni za umma,” amesema Abisai.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kuvuka lengo la kusajili angalau makundi 150 na kutoa zabuni kwa makundi husika. Pia, aliitaka kuongeza bajeti iliyotengwa kwa ajili ya makundi maalum ili ifikie asilimia 30 ya bajeti yake ya ununuzi, hatua itakayoongeza fursa kwa makundi mengi zaidi.

Aidha, ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), iliyowakilishwa na Meneja wa Kanda ya Kati na Magharibi, Mhandisi Suma Atupele, kwa kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023 na kuhakikisha makundi hayo yanasajiliwa ipasavyo katika Mfumo wa NeST.