August 22, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunifu wa dawa salama apunguza uharibifu wa mayai



Na Joyce Kasiki, Tanga
MBUNIFU na mfugaji wa kuku kutoka Mbeya, Nemo Omar, ameibuka na suluhisho linalolenga kupunguza uharibikaji wa mayai wakati wa uangamizaji, kwa kutengeneza dawa ya kunyunyizia mayai inayolenga kuua bakteria na fangasi kabla ya kuwekwa kwenye mashine ya kuatamia.


Omar, ambaye ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), amesema hayo wakati akizingumza na waandishi wa habari kwenye maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Elimu ,Ujuzi na Ubunifu yanayoendelea jijini Tanga viwanja vya shule ya sekondari Usagara jijini Tanga.

Amesema,wazo hilo lilitokana na changamoto ya kupoteza mayai mengi katika mchakato wa kuatamia, hali iliyokuwa ikiathiri shughuli yake ya ufugaji pamoja na wafugaji wengine wadogo.


Amesema mwaka 2023 na 2024 walikumbana na hasara kutokana na mayai kuharibika, huku uelewa alioupata mwaka 2025 kuhusu muundo wa yai ukimsaidia kuelewa sababu mojawapo ya tatizo hilo.


Kwa mujibu wa Omar, ganda la yai lina matundu madogo yanayowezesha kubadilishana hewa, lakini pia yanaweza kuruhusu vijidudu kama bakteria na fangasi kuingia ndani ya yai endapo usafi na utunzaji hautazingatiwa.


“Ukipata yai linatoa harufu, mara nyingi ni dalili kwamba bakteria au fangasi wameingia ndani na kuanza kuliharibu,” amesema Omar.


Amesema baada ya kubaini changamoto hiyo, alitafuta namna ya kuua vijidudu hivyo kabla ya mayai kuwekwa kwenye mashine ya kuatamia.

Kwa sasa, amesema wamebuni dawa inayonyunyiziwa kwenye mayai kabla ya kuanza mchakato huo.


Omar amesema teknolojia ya kutumia kemikali kudhibiti vijidudu kwenye mayai si mpya, akitolea mfano matumizi ya formalin katika baadhi ya uzalishaji wa kuku wa kibiashara.

Hata hivyo, amesema matumizi yake kwa wafugaji wadogo yanaweza kuwa changamoto kutokana na hitaji la utaalamu, maandalizi maalumu na tahadhari za kiafya.


“Tumelenga kutengeneza kitu ambacho ni rahisi kutumia kama maji, lakini kinafanya kazi ya kuua vijidudu bila harufu,” amesema.


Ameongeza kuwa dawa hiyo inalenga kuwapa wafugaji wadogo, hata wanaofuga kuku wachache majumbani, njia rahisi ya kutibu mayai kabla ya kuyaatamisha.


Hata hivyo, Omar amesisitiza kuwa dawa hiyo haiwezi kufanya kila yai litotolee kifaranga, kwa kuwa kazi yake kuu ni kupunguza au kuua vijidudu vinavyoweza kusababisha yai kuharibika, na si kuhakikisha kila yai lina uwezo wa kutotolewa.


Amesema ubunifu huo umeanza kupata msukumo zaidi baada ya kupata usaidizi kupitia Kituo cha Ubunifu na Ujasiriamali cha serikali, KOS-Esik, ambacho amesema kimempa fursa ya kuendeleza ubunifu huo na kupanga namna ya kuwafikia wafugaji wengi zaidi nchini.


Kwa sasa, amesema bidhaa hiyo bado haijaanza kusambazwa rasmi katika maduka, lakini anaamini usaidizi alioupata utasaidia kuifikisha sokoni na kuwafikia wafugaji wengi.


Omar amesema anapatikana Mbezi, Yunga, karibu na eneo la Chuo cha Musi, na kupitia ukurasa wa TikTok unaohusiana na shughuli za ufugaji wa kuku, ambako pia huonyesha shughuli zake za ufugaji na ujenzi wa mabanda.