August 20, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkenda:Ubunifu uzalishwe bidhaa ulete fursa za biashara



Na Joyce Kasiki, Tanga


WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema Serikali inalenga kuhakikisha ubunifu unaofanywa na Watanzania unavuka hatua ya kuonyeshwa kwenye maonesho na kuingia katika uzalishaji wa bidhaa zenye tija kiuchumi.


Profesa Mkenda ameyasema hayo Agosti 18, 2026, wakati akizindua rasmi Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, jijini Tanga.


Amesema Serikali imeendelea kushuhudia matokeo chanya kupitia mashindano ya ubunifu, ambapo baadhi ya wabunifu wamefanikiwa kubadili mawazo yao kuwa bidhaa zinazouzwa na kuwa chanzo cha kipato.


Miongoni mwa bunifu hizo ni mashine za kukamua mafuta ya parachichi, mabegi ya shule yanayotumia nishati ya sola, vifaa maalumu kwa wanafunzi wenye ulemavu, teknolojia za kuchakata chakula cha mifugo pamoja na mita janja za maji.


Kwa mujibu wa Profesa Mkenda, Serikali inafuatilia takribani bunifu 70 zilizo katika hatua tofauti za maendeleo na inaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali pamoja na sekta binafsi ili kuzifikisha katika hatua ya uzalishaji na biashara.

.
“Lengo ni kuhakikisha bunifu hazibaki kwenye maonesho pekee, bali zinakuwa bidhaa zinazotumika na kuleta matokeo kwa jamii na uchumi,” amesema.


Ameongeza kuwa hadi sasa halmashauri 90 zimeanzisha Madawati ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, huku mpango ukiendelea wa kuhakikisha huduma hizo zinapatikana katika halmashauri zote nchini.


Serikali pia, kwa kushirikiana na Benki ya CRDB, imeweka utaratibu wa kuwawezesha wabunifu kupata mitaji ya kuendeleza shughuli zao. Aidha, imeendelea kutumia fursa ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi katika kutafuta masoko, utaalamu na uwekezaji kwa ajili ya bunifu zinazozalishwa nchini.


Akizungumza katika maonyesho hayo Afisa Uhusiano Mwandamizi kutoka Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim (CFR),Maryciana Mhagama, amesema Tanzania inaendelea kutumia Diplomasia ya Uchumi kama nyenzo ya kukuza nafasi ya nchi katika biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kimataifa.


Mhagama amesema hayo wakati CFR ikishiriki katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu inayoendelea katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, Tanga.


Amesema Diplomasia ya Uchumi inalenga kutumia fursa zinazopatikana kupitia mahusiano ya uwili, kikanda na kimataifa, ikiwemo fursa zinazotokana na maeneo huru ya biashara barani Afrika.


“Pamoja na mambo mengine, Uhusiano wa Kimataifa umeweka msisitizo katika Diplomasia ya Uchumi, Uwekezaji, ukuaji wa Biashara, Mikutano, Utamaduni na Utalii,” amesema.


Mhagama amesema CFR pia inaendelea kutoa mafunzo kwa vijana wa Kitanzania kwa lengo la kuwaandaa kuwa wataalamu wenye weledi, wazalendo na wenye uwezo wa kushiriki katika maendeleo ya Taifa.


Amesema kituo hicho hutoa mafunzo katika maeneo mbalimbali, yakiwamo Uhusiano wa Kimataifa, Diplomasia, Menejimenti ya Uhusiano wa Kimataifa, Utawala wa Kimkakati na Diplomasia ya Uchumi.


Aidha, amesema CFR imeandaa mafunzo ya Diplomasia, Itifaki na Ustaarabu (Diplomacy, Protocol and Etiquette) yatakayofanyika kuanzia Agosti 24 hadi 28, 2026, katika kituo hicho jijini Dar es Salaam.


Amewahimiza wadau kutoka taasisi za Serikali na sekta binafsi kutumia fursa hiyo kujiongezea maarifa na ujuzi katika maeneo hayo.