August 19, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Nkasi atatua mgogoro wa ardhi uliodumu miaka 40

Na Israel Mwaisaka, Nkasi

Mkuu wa Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, Peter Lijualikali, ametatua mgogoro wa ardhi uliodumu kwa takribani miaka 40 katika vijiji vya Msilihofu na Katani, wilayani Nkasi.

Katika hatua hiyo, ameagiza kufutwa kwa hati tatu za umiliki wa ardhi katika Kijiji cha Msilihofu, pamoja na kurejeshwa kwa umiliki wa ekari 150 za mashamba mikononi mwa Serikali ya Kijiji cha Katani.

Ametoa maagizo hayo wakati akizungumza na viongozi wa Serikali za Vijiji vya Msilihofu na Katani, ambapo pia amewaagiza Maafisa Ardhi wa wilaya hiyo kuyapima maeneo yote yenye migogoro na kuhakikisha taratibu za kisheria za umiliki wa ardhi zinafuatwa.

Aidha, ameamuru eneo lenye ukubwa wa ekari 150 katika Kijiji cha Katani kupimwa na hati ya umiliki kutolewa kwa mujibu wa sheria.

Katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya pia ameiruhusu familia ya Mzee Apolonal Mwanaloya kuendelea kumiliki eneo lenye ukubwa wa ekari 60, ambalo lilikuwa katika mgogoro kati ya familia hiyo na uongozi wa Kijiji cha Msilihofu, Kata ya Isale.

Hatua hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa ziara za Mkuu wa Wilaya ya Nkasi za kusikiliza na kutatua migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.