Na Joyce Kasiki, Tanga
MAMLAKA ya Elimu na Ufundi Stadi (VETA) imefikia hatua ya kutengeneza simu yake yenye teknolojia iliyobuniwa na wataalamu wake, huku kifaa hicho kwa sasa kikiwa na uwezo wa kupiga na kupokea simu pamoja na kutuma ujumbe mfupi wa maandishi (SMS).
Akizungumza kuhusu ubunifu huo kwenye maonyesho ya kitaifa ya Elimu,Ujuzi na Ubunifu, Mkufunzi wa VETA Pwani Hamis Salum amesema utafiti huo umefikia mwaka wa pili na bado unaendelea.
Salum amesema simu hiyo imetengenezwa kwa kutumia motherboard yao wenyewe, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kujenga uwezo wa ndani wa kutengeneza simu bila kutegemea teknolojia ya kampuni za nje.
Amesema kwa sasa kifaa hicho bado ni kikubwa ukilinganisha na simu zinazotumika kwa sasa, huku watafiti wakilenga kukipunguza ukubwa na kuongeza huduma nyingine zinazopatikana kwenye simu za kisasa kama Samsung na Tecno na nyinginezo.
“Kwa sasa tunaweza kupiga simu na kutuma SMS, lakini bado hatujafikia malengo yetu,” amesema Salum.
Amesema lengo kuu la utafiti huo ni kutengeneza simu yenye uwezo mpana wa matumizi kama simu za kisasa, huku ikiendelea kutumia teknolojia iliyobuniwa na kutengenezwa na wataalamu wa ndani.
Utafiti huo unaendelea katika hatua mbalimbali za maboresho, huku watafiti wakitarajia kuongeza uwezo wa simu hiyo na kuifanya iwe ndogo, rahisi kubeba na kuwa na huduma zaidi.

More Stories
Serikali:Elimu ya ujuzi yaanza kuzaa matunda
ITA Yatumia Maonesho Kuhamasisha Vijana Kusoma Kodi
COSTECH yaongeza juhudi kuibua bbunifu nchini