August 19, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali:Elimu ya ujuzi yaanza kuzaa matunda



Na Joyce Kasiki,Tanga

SERIKALI imesema mageuzi yanayoendelea katika sekta ya elimu yameanza kuonyesha matokeo chanya, hususan katika kuimarisha elimu ya ujuzi na mafunzo ya vitendo mashuleni.


Kauli hiyo imetolewa leo, Agosti 18, 2026, jijini Tanga na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, wakati akikagua maandalizi ya Mashindano ya Ujuzi 2026 na kutembelea banda la shule za sekondari za mkondo wa amali katika ufunguzi wa Maonesho ya Kitaifa ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara.


Prof. Mkenda amesema uwezo unaoonyeshwa na wanafunzi katika kutekeleza kazi mbalimbali za vitendo, ukiwemo ushiriki wa mabinti katika kazi za kiufundi, ni ishara kuwa elimu ya ujuzi inaanza kuwawezesha vijana kujenga uwezo wa kujitegemea na kujiandaa kwa soko la ajira.


Amesema serikali itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali katika kuandaa na kutekeleza mikakati ya kuimarisha mafunzo ya ujuzi, ili kuwafikia vijana wengi zaidi na kutimiza dira ya taifa ya kukuza ubunifu na ajira kupitia elimu ya vitendo.


Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini China, Dkt. Suleiman Haji Suleiman, amesema baadhi ya kampuni kutoka China zilizoshiriki katika maonesho hayo zimevutiwa na uwezo wa wanafunzi pamoja na ubunifu unaoonekana katika kazi zao.


Amesema kampuni hizo zimeonesha utayari wa kusaidia kutoa fursa za mafunzo kwa wanafunzi wa Tanzania, ikiwemo ufadhili wa mafunzo hapa nchini na nchini China.


Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema mpango huo unalenga kuhakikisha kila mwanafunzi anapata fursa ya elimu inayozingatia uwezo na mahitaji yake, wakiwemo wanafunzi wenye mahitaji maalum.


Amesema mkakati huo unatekelezwa katika ngazi zote za elimu, kuanzia elimu ya awali, msingi na sekondari hadi vyuo vikuu, huku elimu maalum ikiendelea kupewa kipaumbele.


Kwa mujibu wa Prof. Nombo, hatua hizo zinajumuisha kuwa na walimu wenye ujuzi wa lugha ya alama, upatikanaji wa vifaa saidizi pamoja na kujenga mazingira rafiki ya kujifunzia, kwa lengo la kuwawezesha vijana wa Tanzania kutimiza ndoto zao.