August 18, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge wa Kawe aimwagia sifa “MBALAMWEZI”

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Mbunge wa Jimbo la Kawe, Geofrey Timothy, amewataka waigizaji na wadau wa sanaa nchini kuongeza uwekezaji katika sekta hiyo akisema bado kuna pengo kubwa la fursa ambalo likitumika vizuri linaweza kuongeza ajira na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa tamthiliya ya “Mbalamwezi” hapo jana, amesema mafanikio yanayoonekana katika tamthilia zinazotengenezwa nchini yanaonesha kuwa soko la sanaa lina uwezo mkubwa, hivyo wasanii na wawekezaji wanapaswa kuendelea kuingiza fedha katika uzalishaji wa kazi za sanaa.

Amesema uwekezaji mkubwa katika tamthilia na kazi nyingine za sanaa unaweza kuibua ajira kwa watu wengi wanaohusika katika uzalishaji, huku Serikali ikinufaika kupitia kodi na shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Aidha, amesema kuna umuhimu wa kujenga miundombinu ya sanaa kama ilivyo katika nchi kama Nigeria na Marekani, akieleza kuwa ujenzi wa arena kubwa unaotarajiwa kufanyika Kawe utasaidia kuweka mazingira bora kwa shughuli za sanaa na burudani.

Aidha, Timothy amesisitiza umuhimu wa kuwaheshimu na kuwaenzi waigizaji wakongwe waliochangia kukua kwa sanaa nchini, akiwataja akina Mama Tasha na Mama Tekla.

Amesema kuna haja ya kuanzishwa utaratibu wa tuzo maalumu za kuwatambua wasanii hao, hatua ambayo kwa mujibu wake itakuwa sehemu ya kuwatendea haki kwa kazi kubwa waliyoifanya na pia kuhamasisha kizazi kipya kuendelea kufanya kazi bora kwa matumaini ya kutambuliwa na kuenziwa siku zijazo.

Kwa upande wake Mtayarishaji wa filamu ya Mbalamwezi, Diwani viti maalum wilaya ya kinondoni, Councellor Lilian Shirima amesema amewahi kukutana na changamoto ya kushinikizwa kufanya ngono ili apewe nafasi za kuigiza, akieleza kuwa hali hiyo iliwahi kuwa miongoni mwa vikwazo vilivyowakabili waigizaji wanawake katika safari ya kutafuta ajira kwenye sekta ya sanaa.

Amesema waigizaji wanafanya kazi ili kujipatia kipato na kusaidia familia zao, hivyo haikuwa sahihi kutumia nafasi za kazi kama njia ya kuwanyonya.