Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Dar
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameiagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kuanzia jana, kukamata malori yote ya mizigo yanayopaki barabara ya Mandela hususani katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya watembea kwa miguu.
Chalamila ametoa agizo hilo jijini Dar-es-Salaam, wakati wa ziara yake ya kutatua kero za wananchi katika Wilaya ya Temeke mkoa humo,ambapo amesema,malori ya mizigohasa yanayobeba makontena, yamekuwa yakipaki katika maeneo ya watembea kwa miguu kwenye barabara hiyo, hali ambayo imekuwa kero kwa wananchi. Pia amesisitiza kuwa mabasi hayaruhusiwi kupaki katika hifadhi ya barabara.
“Natoa agizo kwa Wakala wa Barabara TANROADS, kuanzia leo, kukamata malori yote ya mizigo ya makontena yanayopaki katika barabara za watembea kwa miguu katika barabara hii ya Mandela. Imekuwa kero kubwa, pamoja na mabasi. Ni marufuku kupaki katika hifadhi ya barabara,”amesema Chalamila.
Chalamila amesema,dereva yeyote atakayepaki lori katika barabara hiyo kuanzia sasa akamatwe, kwa kuwa kufanya hivyo ni kujichukulia sheria mkononi huku akijua kuwa ni kosa kisheria.
Aidha amezionya mamlaka zinazotoa vibali kwa malori ya makontena yanayopaki barabarani, akiziagiza kutotoa vibali ovyo kwa lengo la kukusanya fedha.
Amesema malori yanayotaka kupaki yanapaswa kufuata taratibu na kupata vibali kutoka kwa mamlaka husika.
Wakati huo huo, Chalamila ametoa agizo kwa wamiliki wa bandari kavu zote zilizopo Wilaya ya Temeke kukutana katika kikao cha dharura Jumatano asubuhi, kwa ajili ya kutatua changamoto ya malori kupaki ovyo katika barabara ya Sandali kuelekea Mchicha.
Katika hatua nyingine, akizungumzia barabara ya Tuangoma, Chalamila amempongeza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha zege, akisema miundombinu ya zege hudumu kwa muda mrefu.
Pia amewataka wananchi wa Wilaya ya Temeke jijini Dar-es-Salaam, kudumisha amani, akisisitiza kuwa amani ni tunu ya Taifa la Tanzania.

More Stories
Kijana abuni mfumo kuokoa maisha vivuko vya reli
Serikali kuendelea kuimarisha afua za Ukimwi Nchini
TMDA kushirikiana na Mamlaka ya Dawa Dernmark