Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Tanga
SERIKALI imesisitiza umuhimu wa kujenga rasilimali watu yenye maarifa, ujuzi, uwezo wa kufikiri kwa kina na kubuni suluhisho, ili kuiwezesha Tanzania kufikia malengo ya maendeleo yanayolengwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Miaka 50.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, Profesa Ladslaus Mnyone, wakati wa Kongamano la Elimu, Utafiti, Ujuzi na Ubunifu lililofanyika jijini Tanga ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu.
Profesa Mnyone amesema makongamano hayo hayapaswi kuwa mikusanyiko ya kujadili masuala mbalimbali bila hatua za utekelezaji, bali yanapaswa kuzalisha maazimio yatakayosaidia Serikali kuchukua hatua katika kuimarisha elimu, utafiti, ujuzi, sayansi, teknolojia na ubunifu.
Amesema maoni na mapendekezo yatakayopatikana katika mijadala hiyo yatakusanywa na kuunganishwa katika maazimio yatakayowasilishwa kupitia Technical White Paper kwa viongozi wa Wizara, akiwamo Katibu Mkuu na Waziri, na ikiwezekana kufikishwa katika ngazi za juu zaidi za Serikali.
“Hatuna budi kutoka na maazimio yanayoonyesha hatua tunazopaswa kuchukua kutokana na yale tutakayokuwa tumejadili.
” Hatutaki makongamano haya yaishie kuwa sherehe au mikusanyiko ya kujadili mambo bila utekelezaji,” amesema Profesa Mnyone.
Amesema mpango wa Wizara ni kutumia maadhimisho hayo kujadili kwa kina masuala ya elimu, elimu ya juu, ushirikiano na sekta binafsi, pamoja na sayansi, teknolojia na ubunifu.
Kwa mujibu wa Profesa Mnyone, lengo ni kuhakikisha michango inayotolewa na washiriki inabadilishwa kuwa hatua na utekelezaji wenye matokeo, sambamba na kusaidia utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa kwa miaka ijayo.
Akitoa mada katika kongamano hilo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Dkt. Kelvin Swai, amesema Tanzania inapaswa kuanza sasa kujenga msingi wa maarifa na ujuzi utakaowawezesha watoto waliopo shuleni leo kuwa nguvu kazi yenye uwezo wa kuchangia maendeleo ifikapo mwaka 2050.
Dkt. Swai amesema mwaka 2050 hauko mbali kama inavyoweza kuonekana, kwa kuwa watoto wanaosoma katika madarasa kwa sasa ndio watakaokuwa wahandisi, wajasiriamali, wakulima, wataalamu na viongozi wa Taifa katika kipindi hicho.
Amesema elimu ya msingi inapaswa kupewa kipaumbele kwa kuzingatia siyo tu upatikanaji wa elimu, bali pia kiwango cha ujifunzaji na uwezo wa mwanafunzi kutumia maarifa anayopata kutatua changamoto zinazomzunguka.
“Swali muhimu si watoto wetu wanafika shuleni pekee, bali kama wanajifunza, wanaelewa wanachofundishwa na wanaweza kutumia maarifa hayo kutatua changamoto zinazowakabili,” amesema.
Dkt. Swai amesema Tanzania imepiga hatua katika kuongeza fursa za elimu, uandikishaji wa wanafunzi, ujenzi wa madarasa na miundombinu mingine, lakini hatua hiyo inapaswa kufuatiwa na jitihada za kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa na ujuzi unaoweza kutumika katika maisha halisi.
Amesema mabadiliko ya kasi katika teknolojia, uchumi na mazingira yanaifanya Tanzania kuhitaji vijana wenye uwezo wa kufikiri kwa kina, kutatua matatizo, kuwasiliana, kubuni na kuendana na mabadiliko ya dunia.
Kwa upande mwingine, amesema idadi kubwa ya vijana nchini inaweza kuwa fursa muhimu ya maendeleo ya Taifa iwapo vijana hao watawezeshwa kwa maarifa, ujuzi, maadili na fursa za kutumia uwezo wao.
Ameongeza kuwa elimu haiwezi kutazamwa kama suala la sekta moja pekee, bali ni msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, uongozi na ushindani wa Tanzania katika mazingira ya dunia yanayobadilika kwa kasi.
Amesema mjadala wa mustakabali wa elimu unapaswa kuangalia pia aina ya Mtanzania ambaye Taifa linataka kumjenga na nafasi yake katika kuijenga Tanzania baada ya mwaka 2050.
Kongamano hilo limewakutanisha viongozi wa elimu, wataalamu, walimu, wanafunzi na wadau mbalimbali kujadili namna elimu, utafiti, ujuzi na ubunifu vinavyoweza kutumika kujenga msingi wa maendeleo endelevu ya Tanzania.

More Stories
UDOM yaweka mkazo Ubunifu kukabili changamoto za Taifa
Dkt.Lingwanda apongeza ubunifu wa vijana katika maonesho ya NACTVET
BRELA yawahimiza wabunifu kusajili bunifu zao mapema