Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online , Mbeya
TIMU ya Masandawana FC imeibuka mabingwa wa mashindano ya Tulia Trust Uyole Cup 2026 baada ya kuifunga Airport FC kwa penalti 3-2, kufuatia dakika 90 kumalizika kwa sare ya bila kufungana.
Kwa ushindi huo, Masandawana FC imejinyakulia zawadi ya Sh10 milioni pamoja na kombe, huku Airport FC iliyomaliza katika nafasi ya pili ikipata Sh5 milioni.
Timu hiyo iliibuka mshindi kwenye fainali iliyochezwa Agosti 16, 2026, katika Uwanja wa Mwawiji, Uyole ya Kati, Mbeya, ambapo Masandawana walionesha uwezo mkubwa kabla ya kufanikiwa kutwaa ubingwa kupitia mikwaju ya penalti.

Mbali na zawadi kwa mabingwa na mshindi wa pili, mashindano hayo yalitambua pia wachezaji na wadau waliofanya vizuri, akiwemo mfungaji bora, kipa bora, kocha bora pamoja na kikundi bora cha ushangiliaji.
Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi, Spika Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Uyole, ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson, amesema Taasisi ya Tulia Trust itaendelea kudhamini mashindano hayo.
Amesema licha ya changamoto inayoweza kujitokeza kutokana na upanuzi wa barabara katika eneo la Uwanja wa Mwawiji, taasisi hiyo itashirikiana na Serikali kuhakikisha mashindano yanaendelea kufanyika katika eneo hilo.
“Katika hilo, Tulia tutaendelea kuwa wadhamini, hivyo niwaondoe shaka katika hilo. Lakini uwanja unaweza kugeuka kwa mwaka ujao kutokana na eneo dogo kumegwa kwa sababu ya upanuzi wa barabara. Tutajitahidi kushirikiana na Serikali yetu ili ligi yetu iendelee kupigwa Mwawiji,” amesema Dkt. Tulia.
Aidha, Dkt. Tulia amewapongeza wafanyabiashara wanaotumia fursa inayotokana na mashindano hayo kukuza shughuli zao za kiuchumi, ikiwemo kujimudu kimaisha na kusomesha watoto wao.
Amewataka wafanyabiashara kuendelea kutumia fursa zinazotokana na mashindano hayo kwa ajili ya kuboresha maisha yao.
Kwa upande wake, Afisa Michezo kutoka Tulia Trust, Lugano Mwangosi, amesema mashindano ya Tulia Trust Uyole Cup yalianza mwaka 1992, huku Tulia Trust ikianza kuwa mdhamini wa mashindano hayo mwaka 2020.

Mwangosi amesema Dkt. Tulia amekuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia wananchi, kuibua vipaji vya vijana na kuleta fursa mbalimbali kwa jamii.
Naye Mkurugenzi wa Mashindano wa Yanga, Ibrahim Ahmed, amesema wamefika katika mashindano hayo kwa lengo la kuhitimisha kile walichoanza tangu mashindano yalipoanza.
Amesema vijana zaidi ya sita walioonesha vipaji katika mashindano hayo watapewa fursa ya kufanya mazoezi na timu za vijana za Yanga kwa muda wa mwezi mmoja.
“Kubwa zaidi, tutatoa fursa kwa vijana zaidi ya sita ambao walikuwepo katika mashindano hayo tangu mwanzo, ambao watafanya mazoezi na timu zetu za vijana kwa muda wa mwezi mmoja. Tuliwahi kuwa na kijana mmoja ambaye yupo hapa,” amesema Ahmed.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Mkurugenzi wa Raphael Group, Maisha Ambangile, ambaye pia ni Meneja Uzalishaji wa kampuni hiyo, amesema wataendelea kushirikiana na Dkt. Tulia Ackson katika mashindano yajayo kwa lengo la kuibua vipaji zaidi vya vijana.

More Stories
Katibu Mwenezi Wilaya ya Mkuranga Omari Kisatu atoa maelekezo mazito
EMS yapanua wigo utoaji huduma kidigitali
Maji salama ya wafikia wakazi 22,482