November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwakamo: Tutaendeleza harakati za kupata viwanja vya michezo

Na Omary Mngindo, TimesMajira Online, Mlandizi

MGOMBEA Ubunge Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani, Michael Mwakamo ameahidi kushirikiana na na Mamlaka zinazosimamia Ardhi kutenge maeneo ambayo yatatumika kwa ajili ya shughuli za michezo.

Mwakamo ametoa ahadi hiyo katika eneo la kwa Msagasa, Kata ya Mtongani wakati alipokuwa akikiombea kura Chama Cha Mapinduzi CCM.

Amesema, alipokuwa Mtendaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo Mlandizi alifanikisha kupatikana kwa eneo litalojengwa uwanja wa michezo lakini pia akishirikiana na diwani aliyemaliza muda wake Habiba Mfaramagoha walikutana na familia ya Athumani Mbugulu kuwaomba ardhi hiyo.

Baada ya kuwasilisha maombi yao ili kutaka kubadilisha matumizi ya ardhi ambayo familia hiyo ilikuwa inaitumia kwa ufugaji, walikubaliana na walipatiwa na akiwa na viongozi wenzake waliikabidhi Halmashauri.

“Ninayo furaha kubwa kuona ndoto yangu ya Mlandizi na Jimbo linakuwa na maendeleo imeanza kupata mwanga, namshukuru Mungu kuwa katika eneo la Mtongani nilipigania upatikanaji wa eneo litalotumika kwa ujenzi wa uwanja wa michezo, nitakwenda kulisimamia kwa nguvu kubwa,” amesema Mwakamo.

Katika moja ya mipango yake ya kutaka kufanyika kwa michuano ya Jimbo, ni ile inayolenga kuibua na kuendeleza vipaji kwa vijana lakini pia kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha uwanja huo unatumika kwa malengo husika.

Lakini pia amewaomba wakazi wa Kibaha Vijijini na wadau wa michezo kujiandaa kuleta mashindano mbalimbali jimboni humo ili itumike kuongeza umoja, upendo na mshikamano ukizingatia michezo ina nafasi kubwa katika sekta ya ajira.

“Katika Jimbo letu kuna vijana wenye vipaji vya hali ya juu katika michezo hivyo nami nitahakikisha naunga mkono juhudi hizo kwa kuweka miundombinu rafiki ya kifanimisha hayo,” amesema Mwakamo.